Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduizi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itanufaika kwa kiasi kikubwa kupitia uzoefu uliopo Indonesia hasa kwenye sekta ya Mafuta na Gesi, Uchumi wa Buluu, Kilimo cha zao la Karafuu na Mwani.
Rais Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo (jana) tarehe 8 Sept, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baada ya kuwasili nchini akitokea ziarani Indonesia na Msumbiji.
Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali imewakaribisha nchini wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuangalia maeneo ya Uwekezaji hasa kwenye sekta hizo tatu muhimu ambazo bado zina fursa pana zaidi za kuwekeza.
Amesisitiza kwamba Zanzibar inaendelea kuwakaribisha Wawekezaji zaidi kuwekeza Bandari ya Mangapwani kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi sambamba na kuwa na fursa nyingi kwenye sekta mbalimbali zitakazofanyakazi katika Bandari hiyo.
Akizungumzia suala la mafuta na gesi, Rais Dk. Mwinyi amesema uzoefu iliyonayo Ondonesia kwenye sekta ya uchimbaji wa mafuta na gesi kumeivutia Zanzibar kupata uzoefu huo na tayari imeikaribisha kampuni ya “Peltamina” inayomilikiwa na Serikali ya nchi hiyo kuja kuangalia uwezekano wa uchimbaji wa Mafuta na gesi.
Dk. Mwinyi pia amefahamisha sekta hiyo imepiga hatua kubwa Indonesia kwa kufanya kazi hiyo na nchi mbalimbali duniani.
Kuhusu suala la Karafuu Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeingia makubaliano na Indonesia kuja kuangalia uwezekano wa kuchakata bidhaa za karafuu kwa kuziongezea thamani ili Zanzibar iuze bidhaa hizo badala ya Mali ghafi.
Rais Dk. Mwinyi pia ameeleza mpango wa Serikali kuanzisha vikundi vya Wajasriamali vya akina mama kwa dhamira ya kuwa na vituo vya kuchakata majani ya karafuu.
Kuhusu sekta ya utalii, amesema Serikali ya Indonesia imekubali kutoa fursa za mafunzo kwa vijana wa Zanzibar kwenda Indonesia kujifunza masuala ya Utalii.
Alipowasili Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Rais Dk. Mwinyi alipokelewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha Mapinduzi, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.