Media » News and Events

Zanzibar iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Muuungano wa Visiwa vya Comoro.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk.Hus sein Ali Mwinyi (kulia) akisisitiza jambo wakati akizungumza na Mgeni wake Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Nchini Tanzania Mhe. Dkt.Ahamada El Badoi Mohamed Fakih alipofika Ikulu jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Zanzibar iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Muuungano wa Visiwa vya Comoro hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya biashara.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Dk. Ahamada El Badoi Mohamed Fakih.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Fakih kwamba kutokana kuwepo kwa mahusiano ya kidugu baina ya pande mbili hizo ni kichocheo pekee cha wafanyabiashara wa Zanzibar na Comoro kuimarisha sekta ya biashara hasa kutokana na muingiliano wa kidugu uliopo.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi Fakih kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake itaendeleza na kudumisha uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo sambamba na kuendeleza sekta za uchumi kwa mashirikiano ya pamoja kwa maslahi ya nchi mbili hizo na watu wake.

Nae Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Dk. Ahamada El Badoi Mohamed Fakih alimueleza alimueleza Rais Dk. Mwinyi haja ya kurudisha utamaduni wa wafanyabiashara wa Comoro kuja kufanya biashara Zanzibar na wale wa Zanzibar kwenda nchini Comoro kwa ajili ya kufanya biashara.

Balozi Fakih alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Mwinyi uhusiano na ushirikaiano wa kihistoria uliopo kati ya Comoro na Zanzibar ambao una kila sababu ya kuimarishwa zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Aidha, Balozi Fakih alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya nchi yake ya kutekeleza Mkataba wa Makubaliano yaliyokubaliwa kati ya Zanzibar na Comoro katika uongozi wa Awamu iliyopita huku akitoa shukurani kwa huduma kadhaa wanazozipata wananchi wa Comoro katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo huduma za afya, elimu na nyenginezo.


Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikuna na kufanya mazungumzo na Balozi wa Namibia nchini Tanzania Lebbius Tangeni aliyefika Ikulu kujitambulisha ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao walisisitiza haja ya kuwepo mashirikiano ya pamoja hasa katika uendelezaji wa sekta za kiuchumi ikiwemo viwanda, biashara, uwekezaji pamoja na mahusiano ya Miji na Manispaa za Zanzibar na Namibia.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Tangeni alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua na juhudi za makusudi alizoanza kuzichukua za kuazimia kukutana na uongozi wa ngazi za Mikoa wa Zanzibar pamoja na viongozi wa Manispaa na Jiji la Zanzibar kwa azma ya kuweka mahusiano na ushirikiano kati yao na ndugu zao wa Namibia katika maeneo hayo.

Balozi Tangeni alieleza kwamba mbali ya azma yake hiyo ya kukutana na viongozi hao pia, ana lengo la kukutana na uongozi wa Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), ili kuweza kushirikiana na kuleta mahusiano pamoja kati ya Mamlaka hiyo na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Namibia.

Aidha, Balozi Tangeni alieleza mashirikiano ya kihistoria yaliopo kati ya Namibia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yameasisiwa na viongozi wakuu wa nchi mbili hizo tokea wakati wa kudai uhuru ambayo yanahitaji kuimarishwa zaidi.

Nae Rais Dk. Mwinyi kwa upande wake alimueleza Balozi huyo wa Namibia, Dira ya Serikali anayoiongoza ya Uchumi wa Buluu na kusisitiza kwamba Namibia ina nafasi nzuri katika kushirikiana na Zanzibar kwenye Dira hiyo hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vya samaki.

Mapema, Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jaji Dk. Elieza Mbuki Feliesh ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa na Wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi huku akieleza azma yake ya kuimarisha kada ya Sheria hasa kwa vijana hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi kwa upande wake alimpongeza Jaji Felesh kwa kupata uteuzi huo na kueleza imani yake kwamba kiongozi huyo atafanya kazi kwa ustadi kubwa kutokana na uzoefu alionao huku akieleza muingiliano uliopo kwenye sekta ya sheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unahitajia mashirikiano ya pamoja kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.