Dk. Hussein Ali Mwinyi amemtumia salamu za pole Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknonojia ya Habari Nape Nnauye.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemtumia salamu za pole Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknonojia ya Habari Nape Nnauye kufuatia ajali ya gari iliyotokea Wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu na kusababisha vifo vya watu wakiwemo waandishi wa habari.

 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ametoa salamu hizo za pole kwa ndugu jamaa na marafiki pamoja na wadau wote wa habari.

 

Katika salamu hizo za rambirambi,  Rais Dk. Mwinyi alieleza kusikitishwa na vifo hivyo na kuwanasihi ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wadau wote wa habari kuwa na subira na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha misiba hiyo.

 

Rais Dk. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu mahala pema peponi,  Amin.

 

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi amemuomba MwenyeziMungu kuwaponya kwa haraka wale wote waliopata majeraha kutokana na ajali hiyo.