Dk.Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu waliofariki kufuatia ajali ya basi lililogongana na lori huko katika eneo la Melea, Kibaoni, Mkoani Morogoro.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu waliofariki kufuatia ajali ya basi lililogongana na lori  huko katika eneo la Melea, Kibaoni, Mkoani Morogoro.

 

Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alieleza kusikitishwa na vifo vilivyotokana na ajali hiyo na kuzinasihi familia za marehemu kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha misiba hiyo.

 

“Kwa niaba yangu binafsi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake tunatoa mkono wa pole kufuatia vifo hivyo vilivyotokana na ajali hiyo na tunaungana na ndugu, jamaa na marafiki katika maombolezi”, ilieleza sehemu ya salamu hizo za rambirambi za Rais Dk. Mwinyi.

 

Rais Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu awalaze Marehemu wote mahala pema peponi,  Amin.

 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wa ajali hiyo kupona kwa haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaisha.

 

Ajali hiyo ilitokea jana jioni Machi 18 ambapo watu 22 walifariki dunia huku zaidi ya 30 wakijeruhiwa baada ya basi lenye namba za usajili T732 ATH mali ya Kampuni ya AHMEED linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Tanga kugongana uso kwa uso na lori lenye namba IT 2816 katika eneo la Melea, Kibaoni barabara ya Iringa-Morogoro.