Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kilele cha Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI, KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 58 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

TAREHE: 11 JANUARI, 2022

 

Assalamu Aleikum

Tunamshukuru Mwenyezi Mtukufu, Mwingi wa Rehma kwa kutujaaliya uhai na afya njema na kutuwezesha kufikia siku ya leo, tukielekea katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 12 mwaka 1964 yatakayofanyika kesho tarehe 12 Januari, 2022 katika uwanja wa Amani.

 

Tunasherehekea na kuadhimisha kutimia miaka 58, tangu wananchi wa Zanzibar tulipojikomboa na kuondokana na unyonge wa kutawaliwa kwa miongo kadhaa. Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni mwanzo wa safari ya maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar kwa kupata mamlaka ya kujiamulia wenyewe mambo yetu ya msingi kwa mustakabali wa maisha yetu.

 

Ni dhahiri kuwa, mafanikio tuliyoyapata katika sekta mbali mbali kwa kipindi cha miaka 58, yametokana na uongozi thabiti wa Waasisi wa Taifa letu na viongozi wote wa awamu za Uongozi zilizotangulia. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunayalinda na kuyadumisha Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Tanzania tukijuwa kwamba hizi ni tunu muhimu tulizoachiwa na waasisi wetu.

 

Ndugu wananchi,

Tunapoadhimisha siku ya Mapinduzi kila mwaka, tuna wajibu wa kuwakumbuka Waasisi wetu wakiongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wetu wote waliotangulia mbele ya haki, ambao walijitoa muhanga kwa ajili ya Taifa letu na kuitumikia nchi yetu kwa moyo, ujasiri na uzalendo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi. Na wale walio hai, Mola awape afya njema na umri mrefu tuendelee kunufaika kwa hekima na busara zao katika safari yetu ya maendeleo.

 

Haya ni Maadhimisho ya pili kwangu tangu kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mwaka jana nilieleza kwamba sote tuna kazi ya kutafsiri kivitendo Malengo ya Mapinduzi kwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kustawisha maisha ya Wazanzibari. Tumedhamiria kushirikiana kujenga uchumi mpya wa Zanzibar kwa umoja, mshikamano na maridhiano ili kila Mzanzibari apate fursa ya kuchangia maendeleo na kunufaika na matunda ya Mapinduzi kwa misingi ya usawa.

 

Katika shamra shamra za Maadhimisho haya ya miaka 58 ya Mapinduzi yenye kaulimbiu;” Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo Endelevu”, jumla ya miradi 30 imefunguliwa na 13 imewekewa mawe ya msingi. Nawashukuru sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika shughuli zilizopangwa ikiwa ni ishara nzuri za kuunga mkono jitihada zetu za kuleta maendeleo.

 

Ndugu Wananchi,

Kwa hakika, miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kipindi kirefu. Katika kipindi hicho tumepata mafanikio mengi na vile vile tumekabiliana na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo.

 

Ni utamaduni uliojengeka na tuliourithi kutoka kwa viongozi wa Awamu zilizopita, kutumia sherehe za Mapinduzi kwa kutathmini na kutafakari mafanikio tuliyoyapata katika kujenga nchi yetu pamoja na kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano.  Vile vile, huwa tunatumia wakati huu kwa kuzitathmini changamoto mbali mbali zilijitokeza kwa nyakati tofauti   na kupanga mikakati ya kuzitafutia ufumbuzi. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane itaendeleza utamaduni huu muhimu kwa maendeleo yetu.

 

Kwa msingi huo, ni vyema tukaendelea kutathmini maendeleo tuliyoyapata katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020, MKUZA Awamu ya 3, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 pamoja na Mipango ya maendeleo ya Kimataifa katika mwaka 2021 uliomalizika.

 

 

AMANI NA UTULIVU

Ndugu wananchi,

Moja ya mafanikio tuliyoyapata na tunayopaswa kujivunia ni kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano. Kwa hakika hii ndiyo misingi muhimu inayotuwezesha kuzidi kupiga hatua katika sekta zote za maendeleo.

 

Natoa shukrani zangu za dhati kwa viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na asasi za kiraia, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae. Nawahakikishia wananchi na wageni wote wanaotutembelea kwamba, nchi yetu ipo salama na kwamba Serikali zetu zote mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria katika kulinda amani, utulivu na maisha ya wananchi wote na mali zao.

 

UCHUMI

Ndugu Wananchi,

Kuwepo kwa hali ya amani na ya utulivu kumetuwezesha kutekeleza mipango yetu ya maendeleo, ingawa sio kwa kasi tuliyoitarajia kutokana na kuwepo kwa janga la maradhi ya UVIKO- 19, ambalo limeathiri sana hali ya kiuchumi ya mataifa yote duniani.

Katika mwaka 2021, kasi ya ukuaji wa uchumi iliimarika ikilinganishwa na mwaka 2020, ambapo athari za Maradhi ya UVIKO, zilikuwa kubwa zaidi. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 (Januari – Machi) uchumi wa Zanzibar ulikuwa kwa wastani wa asilimia 2.2 ikilinganishwa na asilimia 1.8 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2020. Kwa kipindi cha robo ya pili (Aprili – Juni) uchumi umeendelea kuimarika zaidi na kufikia ukuaji wa wastani wa asilimia 6.5 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 1.4 kwa kipindi kama hicho mwaka 2020. Katika robo ya tatu ya mwaka 2021, (Julai – Septemba) uchumi wetu ulikua kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na asilimia 3.3 kwa kipindi kama hicho katika mwaka 2020. Ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji, kuimarika sekta ya utalii pamoja na shughuli za biashara.

Juhudi kubwa zimefanywa na Serikali za kudhitibiti mfumuko wa bei, ikiwa ni pamoja na kuweka bei elekezi kwa baadhi ya bidhaa muhimu. Kasi ya mfumuko wa bei kwa kipindi cha Januari – Novemba 2021 ilifikia wastani wa asilimia 1.7 ikilinganishwa  na wastani wa asilimia 3.4 kwa kipindi kama hicho cha mwaka 2020.

 

Ndugu wananchi,

Kwa kipindi cha Januari- Novemba 2021, Serikali ilikusanya jumla ya Shilingi billioni 745.1, sawa na ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi bilioni 610.5 zilizokusanywa kwa kipindi cha Januari – Novemba 2020. Ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa uchumi pamoja na kuanza kutumika kwa mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato iliyoanzishwa. Mifumo hiyo inaziunganisha taasisi mbali mbali za Serikali, baina ya Taasisi za Serikali na Wafanyabiashara.

 

Vile vile, Serikali imefanya marekebisho ya sheria za kanuni za kodi kwa lengo la kuondoa malalamiko ya kuwepo kwa utitiri wa kodi na ada. Ni matumaini yangu kwamba, hatua hiyo itashajiisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kukuza ajira na kuongeza usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

 

Vile vile, marekebisho ya sheria tuliyoyafanya yamesaidia kutoa unafuu wa ushuru wa stempu kwa wafanyabiashara wadogo na wakati kwa kupunguza viwango maalum kutoka Shilingi 200,000 hadi Shilingi 100,000, kutoka Shilingi 732,000 hadi Shilingi 200,000 pamoja na kupunguza kiwango cha ushuru wa stempu kutoka asimilia 3 hadi asilimia 2 kwa mwaka.

 

UWEKEZAJI

Ndugu Wananchi,

Kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Disemba 2021, Serikali kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA),  imesajili jumla ya miradi 120 yenye mtaji wa Dola za Kimarekani Milioni 787. Miradi hiyo inatarajiwa kutoa zaidi ya ajira elfu 7. Tayari wawekezaji wamejitokeza katika visiwa 10 vilivyotangazwa kukodishwa. Jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 261 zitawekezwa kwenye visiwa hivyo ikiwa ni uwekezaji wenye hadhi ya juu.

Download File: