Taarifa kwa vyombo vya Habari.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, leo tarehe 7 Oktoba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi Afrika (BADEA), Dk. Sidi Ould Tah.

Mhe. Rais ameupongeza uamuzi wa Benki hiyo wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya Elimu na Afya huku akitumia fursa hiyo kuipongeza mikakati ambayo benki hiyo imeiweka katika kusaidia sekta ya Kilimo, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na kuwasaidia Vijana na Wanawake.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Dk. Sidi Ould Tah amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Benki hiyo itaendelea kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kufikia malengo yake iliyojiwekea hasa katika Kipaumbele cha Sera ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Dira ya Uchumi wa Buluu.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi amekutana na kuzungumza na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu Jaji Imani Daudi Aboud na kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo huku akiahidi kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kutekeleza majukumu yake.

Rais Dk. Mwinyi amemueleza Jaji Imani Aboud kwamba hivi sasa Zanzibar ina Amani, Usalama na Utulivu wa kutosha, hatua ambayo imezidi kuimarika kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa upande wake Jaji Imani Daudi Aboud amemtaarifu Mhe. Rais Dk. Mwinyi kuwa malengo na majukumu ya Mahakama anayoiongoza ni pamoja na kulinda na kudumisha haki za binaadamu na watu katika mataifa yote ya bara la Afrika.

Download File: