Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi amewaonya wafanyabiashara visiwani Zanzibar wanaopandisha bei ya bidhaa muhimu kwa kizingizio cha athari zitokanazo na uginjwa wa Uviko-19 maarufu kama Corona.

Alhaj Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waumini wa Kiislam mara baada ya sala ya Ijumaa katika msikiti wa Noor Al Abswar maarufu msikiti wa Abdallah Rashid, Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

“Kibaya zaidi kuna baadhi ya bidhaa wala hazitoki China na Ulaya lakini bidhaa inakuwa juu. Leo kuna saruji inayatoka Dar es Salaam na Mtwara kuna sababu gani kufika elfu 20? Kwa hivyo, Nawataka wafanyabiashara wasipandishe bei za bidhaa hovyo wanawaumiza watu.” Alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Aidha, Alhaj Mwinyi, ameitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kusimamia upandishwaji holela wa bei za bidhaa muhimu ili kuwapatia unafuu wananchi na watumiaji wa mwisho.