RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewasisitiza wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendeleza mshikamano, umoja pamoja na amani iliyopo.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati akiwasalimia wananchi wa Mwanza pamoja na Watanzania wote waliohudhuria katika maadhimisho ya Sherehe za miaka 58 ya Uhuru na miaka 57 ya Jamhuri ya Tanzania Bara zilizofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Katika salamu zake hizo Rais Dk. Shein alieleza kuwa mshikamano, umoja na amani iliyopo hapa nchini ndio msingi pekee wa maendeleo ya Watanzania wote.

Rais Dk. Shein aliungana na viongozi wengine wa Tanzania wakiwemmo Marais wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu pamoja na viongozi wa vyama vya siasa ambao walipewa nafasi ya kusalimia na Rais Magufuli katika uwanja huo ambapo Rais Dk. Shein nae alisisitiza suala zima la amani hapa nchini.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wa Tanzania kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwani anafanya kazi nzuri kwa kila sehemu ya Tanzania ambapo kila mmoja anaiona.

Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapa salamu wananchi wa Mwanza zinazotoka kwa ndugu zao wa Zanzibar na kuwaeleza kuwa Wazanzibari wote wako pamoja na ndugu zao wa Tanzania Bara katika kusherehekea siku yao hii adhimu na muhimu ya uhuru kwani hio ni sherehe yao wote.

Nao badhi ya viongozi wakuu waliofika katika sherehe hizo wakiwemo Marais wastaafu, Mawaziri wakuu wastaafu pamoja na viongozi wa vyama mbali mbali vya siasa hapa nchini walitumia fursa hiyo kwuasalimia wananchi wa Mwanza.

Mapema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli aliwahutubia wananchi na kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana ndani ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Sambamba na hayo alieleza mikakati aliyowekwa na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha uchumi unazidi kuimarika.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kwa uwezo aliopewa Kikatiba kwa kutoa msamaha kwa wafungwa wapatao 5533 walioko magereza mbali mbali katika Mikoa ya Tanzania Bara huku akiagiza kufanywa haraka kutolewa ili warudi uraiani.

Akieleza kuhusu msamaha huo Rais Magufuli aliwataka wale wote watakaopata msamaha huo kujutia makosa yao waliyoyafanya na kumshukuru Mungu huku akisisitiza kuwa msamaha huo isiwe sababu ya kurejea kufanya tena makosa kwani adhabu kali itatolewa kwa watakaopata msamaha na baadae kurejea tena makosa yao.

Rais Magufuli alitoa pongezi kwa wananchi wote waliohudhuria sherehe hizo ambao walitia for a uwanjani hapo kutokana na maelfu ya wananchi wa Mwanza na mikoa ya jirani kuhudhuria pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na Mabalozi na wakuu wa Mashirika ya Kimataifa.

Sherehe hizo zilipambwa na Gwaride ambalo lilitoa salamu ya Rais na kupita mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa mwendo pole pamoja na mwendo wa haraka, mizinga 21 ilipigwa pamoja na wimbo wa Taifa na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zilipigwa na kuimbwa.

Matukio mengine ambayo yaliwafurahisha wananchi waliofika uwanjani hapo ni pamoja na onyesho la ndege za kivita, onyesho la Kwata ya Kimya kimya, onyesho la Helikopta, onyesho la gari ya Zimamoto ya Nyumbu, onyesho la Sungusungu pamoja na vikundi maalum vya ngoma za asili ambazo zilitumbuiza.