WAZANZIBARI wametakiwa kuthamini na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusimamia na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, hatua inayotowa fursa kwa waumini kuweza kuabudu bila taabu.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kijiji cha kulelea watoto cha SOS kiliopo Mombasa Asha Salim Ali, alipotowa shukrani baada ya hafla ya Futari, iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mwanamwema Shein na Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Suleiman Idd kwa ajili ya watoto wa Kijiji hicho.

Mkurugenzi huyo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein kwa juhudi kubwa inazoendelea kuchukuwa kudumisha na kuendeleza amani na utulivu nchini.

Aliipongeza Serikali kwa kujali na kutambua mazingira ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hivyo kuwa karibu nao na kuwasaidia muda wote.

Aidha, aliipongeza Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, wanwake na watoto kwa kjusimamia kikamilifu haki za watoto, ikiwemo yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Alisema Bodi,  Uongozi na watoto wa Kijiji hicho wamefarijika na hatua ya viongozi hao ya kuendeleza utamaduni wa kuwafutarisha kila mwaka, hatua inayojenga imani na mapenzi makubwa kwao.

Aidha,  alitowa pongezi kwa kukiteuwa kijiji hicho kuwa cha kwanza kuandaliwa futari mwaka huu na kutowa shukurani kwa waandaaji wa futari hiyo pamoja na kuwatakia Afya njema na maisha marefu.