RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliwaongoza Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi mbali mbali katika Maulidi ya kuadhimisha Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kitaifa yaliofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.
Sherehe hizo za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar ambao huungana na Waislamu wenzao wote duniani ambapo kwa hapa nchini zilianzishwa mapema mnamo mwaka 1926.
Alhaj Dk. Shein aliungana na Waislamu pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na viongozi wa Dini na wananchi ambapo pia, Mama Mwanamwema Shein nae alihudhuria Maulid hayo akiwa pamoja na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa.
Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote pamoja na viongozi mbali mbali waliohudhuria katika Maulid hayo akiwemo Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ambae pia, ni mlezi wa Jumuiya ya Milade e Nabii ambayo inasimamia shughuli za Maulid ya kitaifa hapa nchini.
Katika Sherehe hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.
Akisoma khutba ya Maulid hayo, Sheikh Hassan Ali Kombo kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana alisema kuwa kila Muislamu inampasa kumpenda Mtume Muhammad (S.A.W) yeye na kizazi chake huku akisisitiza haja ya uendeleza utamaduni huo ambao umekuwa ukitumika kwa muda mrefu hapa Zanzibar.
Aidha, Sheikh Hassan aliwataka Waislamu kuwa kitu kimoja na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha umoja na mshikamano kwa lengo la kupata rehema za Allah.
Sheikh Hassan pia, alitumia fursa hiyo kukemea mambo maovu katika jamii hasa suala la unyanyasaji wa wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na suala zima la ubakaji jambo ambalo limeshamiri hivi sasa katika jamii na kueleza athari zake na kutaka mashirikiano ya pamoja katika kulipiga vita.
Aidha, alieleza kuwa ni jukumu la Waislamu kusherehekea siku hii adhimu pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu, kufuata kitabu chake cha Qur-an pamoja na kufuata mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W) aliyokuja nayo.
Mapema Mshauri Mkuu wa Kamati ya Maandalizi wa Jumuiya ya Milade e Nabii ambayo inasimamia shughuli za Maulid ya kitaifa hapa nchini Sheikh Sherali Champsi alieleza historia ya Maulid hapa Zanzibar ambayoinatimiza miaka 94 tokea kuanzishwa kwa shughuli hizo hapa nchini.
Sherehe hizo za Maulid ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na Ustadhi Miraji Nyange Khamis kutoka Kigunda Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo tafsiri yake ilitolewa na Sheikh Ilyasa Hassan Hamad kutoka Chuo cha Kislamu Mazizini mjini Unguja.
Milango ya Maulid Barzanji iliyoenda sambamba na Qasweeda ilisomwa na Maustadhi kutoka vyuo mbali mbali vya Qur-an kutoka Unguja na Pemba yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni, Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo adhimu.
Katika sherehe hizo za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Madrassa Noor El Islamiya ya Mji Mkongwe, Mjini Unguja ilisoma Qiyaam Talaa, kilichotanguliwa na Mlango wa nne uliosomwa na Ustadhi Juma Faki Omar kutoka Amani, Mjini Unguja.
Qasweeda ya mwaka 1441 Al Hijra, ilisomwa na wanafunzi kutoka Madrassa Munawara ya Shaurimoyo, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulid hayo Sheikh Sherali Chapsi alitumia fursa hiyo kama ilivyokaida kwa kila mwaka kumkabidhi Rais, Qasweeda hiyo maalum.
Maulid hayo yalimalizika kwa Mlango wa dua uliosomwa na Abubaker Said Abubaker, kutoka Mji Mkongwe Unguja na hatimae kufungwa kwa fatha iliyosomwa na Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi chini ya mshereheshaji Mohammed Suleiman (Tall).