RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar amesisitiza kwamba ataendelea kuwathamini Wazee wa CCM kwani walikuwa na mchango mkubwa katika uongozi wake Serikalini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipozungumza na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutoka Unguja na Pemba ambao walifika Ikulu kwa ajili ya kumuaga sambamba na kumpongeza kwa uongozi wake uliotukuka wa miaka kumi ya Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa katika maisha yake ya uongozi Serikalini Wazee wa CCM walimpa ushirikiano mkubwa hali iliyopelekea Zanzibar kupata mafanikio hivyo ataendelea kuwajali na kuwathamini.
Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee wa CCM ndio njia yake ya uongozi kwani aliishi nao vizuri kwa kutambua mchango wao mkubwa katika Taifa hili.
Aliongeza kuwa wazee wana nafasi kubwa katika jamii kutokana na silka na tamaduni ziliopo hivyo, kuna kila sababu ya kuendelea kuwatunza na kuwaenzi sambamba na kuwaheshimu wazee.
Alisema kuwa wazee wa CCM aliweza kuishi nao na kufanya kazi zao vizuri katika uongozi wake jambo ambalo lilimpa faraja na kuweza kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika vipindi vyake vyote viwili vya uongozi na kupata mafanikio makubwa.
Aidha, Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa kuweza kufanya kazi na wazewe hao kwa kipindi kirefu kwani anatambua kwamba kuthaminiwa kwa wazee hao ni sawa na kuyathamini na kuyatunza Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.
Alieleza kuwa wazee hao wameshiriki kikamilifu katika ukombozi wa Zanzibar hivyo, si jambo la busara wakadharauliwa na ndio maana katika uongozi wake aliwapa kipaumbele wazee wote wa Unguja na Pemba tena bila ya ubaguzi.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwahakikishia wazee hao wa CCM kuwa ataendelea kukitumikia chama hicho hata baada ya kustaafu katika wadhifa wake wa Urais wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza amani, utulivu na umoja miongoni mwa wananchi wa Zanzibar huku akiwaeleza wazee hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga vyema katika kukabiliana na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka huu.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Zanzibar Bi Khadija Jabir Mohamed alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwafanyia mema mengi wazee hao wa CCM pamoja na wazee wote wa Zanzibar.
Mapema Katibu wa Baraza hilo la Wazee Zanzibar Waziri Mbwana Ali akisoma risala ya wazee hao alisema kuwa Rais Dk. Shein amechukua jitihada kubwa ya kufanya kazi vizuri na kufanikisha maendeleo ya Zanzibar ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.
“Tunakiri wa dhatyi ya nyoyo zetu kwamba umekitendea haki Chama Cha Mapinduzi, umewatendea haki Watanzania walio wakaazi wa Zanzibar wakiwemo wazee waliokuchagua kwa jinsi ulivyotekeleza kikamilifu ahadi za kuwatumikia wananchi”, walieleza wazee hao.
Aidha, wazee hao walieleza kuwa katika vipindi vyake viwili vyua uongozi wazee wameshuhudia jitihada alizozichukua katika kutekeleza ahadi moja baada ya nyengine kwa kuweza kuzitatua changamoto mbali mbali na kuweza kuzitatua kwa ushirikiano na viongozi wenzake na wananchi.
Walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika kipindi chake cha mwanzo cha uongozi wakati akiingia madarakani bila kuyumba huku akiamini kwamba uvumilivu na ustahamilivu ndio misingi ya utekelezaji wa demokrasia.
Wazee hao walieleza kuwa uchumi wa Zanzibar umeweza kukua na hivyo kurahisisha utekelezaji wa matakwa ya wananchi kwenye sekta za huduma za wananchi na kusema kuwa wao wazee pamoja na wananchi wanafarajika na kufurahia maendeleo wanayoyaona.
Wakati huo huo, wazee hao walimkabidhi Rais Dk. Shein zawadi pamoja na Jarida maalum lenye kueleza shukurani kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanyika katika uongozi wa Rais Dk. Shein.