RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo amewaapisha watendaji mbali mbali wa Serikali kushika nyadhifa zao baada ya kuwateua hivi karibuni.Katika hafla hiyo iliofanyika Ikulu Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Mgeni Jeilani Jecha kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) pamoja na kumuapisha Valentine Andrew Katema kuwa Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar.
Aidha, alimuapisha Shaheen Fauz Mohammed kuwa Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali.
Hafla hiyo ya kiapo ilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said pamoja Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Mwinyi Talib Haji.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wanafamilia.
Wakizungumza baada kiapo hicho, watendaji hao walimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaamini na kuwateua kushika nyadhifa hizo na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi na mashirikiano.
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Mgeni Jeilani Jecha alisema ameazimia kuwahudumia wananachi wote kwa haki na usawa kwa kufuata Katiba ya Zanzibar na kuahidi kuweka mikakati maalum ya kukabiliana na wimbi la makosa ya jinai, hususan kesi za Udhalilishaji wa kijinsia.
Aliwataka wananchi kuwa na imani na Ofisi hiyo, huku akibainisha azma yake ya kuweka mikakati ya kuwashirikisha wananchi ili waweze kuwa na mwamko wa kufika mahakamani kutoa ushahidi.
Alisema atahakikisha anajenga mashirikiano ya karibu kati ya Ofisi ya DPP na wadau wengine wa masuala ya sheria ikiwemo Jeshi la Polisi, mahakama pamojana Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA)