Dk. Shein amesema kuwa hatua hiyo ni pamoja na kuondosha ada kwa akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua katika hospitali zote za Serikali ikiwemo hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.Alisisitiza kuwa haiwezekani na hakuna sababu ya msingi ya kuwachangisha akina mama wajawazito Shilingi arobaini elfu kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua.Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kushindwa kuchangia mchango huo kwa akina mama wajawazito kwani mchango huo hauna tija kwa Serikali na wala sio mchango wenye kiasi kikubwa cha fedha.Alisema kuwa hoja kubwa ni kupunguza matatizo ya wazazi wanayopata wakati wa kujifuangua ikiwemo vifo,  huku Serikali ikiwa na lengo la kufikia Milenia katika sekta ya afya, hivyo imeamua kwa makusudi kutowatoza fedha akina mama hao na fedha zote italipa Serikali yenyewe.“Hivyo niulize ndugu zangu tukiwaambia wazazi wachangie elfu arobaini ndio tunawasaidia hivyo?...... mimi nimeamua hili tuliondoshe kabisa”,alisisitiza Dk. Shein,Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kina mama wote ni lazima watambue hilo na Serikali italitilia mkazo na mwaka huu itaongeza fedha za dawa, vifaa ili huduma ziweze kuimarika na kupunguza utegemezi kutoka kwa wahisani.Dk. Shein ameeleza kuwa imefika wakati Zanzibar ianze kujitegemea na kuepuka kukaa pembeni na kuwasubiri wahisani kwani kuna siku wanaweza kusema hawana na badala yake kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.“Ni vizuri tuanze wenyewe, tusisubiri wahisani, hivi sasa tumefika pazuri kutokana na hali yetu ya uchumi ilivyo…..Zanzibar tunakopesheka kwa kiasi kikubwa kwani uwezo upo”,alisema Dk. Shein.Akieleza ombi alilopewa na wakulima wa bonde la mpunga la Muyuni B, la kutaka wapatiwe kinu cha kusagia mpunga, alisema kuwa Serikali haishindwi na kueleza kuwa tayari ameshamuagizia Katibu Mkuu Wizara ya kilimo kutafuta kinu kilichobora na madhuti ambacho kitadumu muda mrefu na kueleza kuwa hata yeye anaweza kununua kinu hicho kwa fedha zake mwenyewe.