RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya India Shri Ram Nath Kovind kwa kuadhimisha siku ya Jamhuri ya Taifa hilo ambayo huadhimishwa kila ifikapo Januari 26 ya kila mwaka.
Katika salamu hizo za pongezi zilizotumwa na Rais Dk. Shein zilieleza kwua kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar pamoja na yeye mwenyewe binafsi ana furaha na anaungana pamoja na kiongozi huyo, wanafamilia na wananchi wote wa India katika kusherehekea siku hii adhimu.
Rais Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa Zanzibar na India zina uhusiano wa kihistoria na udugu wa damu pamoja na kuwa na uhusiano wa kiuchumi na kuelezaa kuwa mafanikio makubwa yaliopatikana India yamepelekea nchi hiyo kuimarika kiuchumi sambamba na wananchi wake kuendelea kupata mafanikio.
Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa hatua hiyo inadhidisha na kujenga thamani ya mahusiano kati ya India pamoja na Serikali ya Mapinduzi ua Zanzibar na watu wake.
Kutokana na juhudi hizo zinazochukuliwa na pande mbili hizo katika kukuza uhusiano na ushirikiano yaliopo, salamu hizo za Rais Dk. Shein zilisisitiza haja ya kuzidisha na kuiimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano ya kiuchumi kwa lengo la kuleta manufaa kwa nchi mbili hizo pamoja na watu wake.
Rais Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo yeye, familia yake pamoja na wananchi wa Jamhuri ya India kusherehekea vyema siku hiyo adhimu sambamba na kusherehekea kuingia kwa mwaka mpya wa 2020 wakiwa na afya njema pamoja na furaha, heri na fanaka tele.
India ilipata Jamhuri yake mnamo Januari 26 mwaka 1950 baada ya kupata uhuru kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza mnamo mwaka 1947 chini ya uongozi wa muasisi na Baba wa Taifa hilo Hayati Mahtma Gandi.