Katika hotuba yake Dk.Shein alieleza kuwa katika kufanikisha jambo hilo, ni lazima Chuo hicho kiwe karibu na Tume ya Mipango ili kuona maeneo ambayo inapaswa kuyazingatia katika fani zinazotolewa Chuoni hapo.Alisema kuwa umefika wakati Chuo kijielekeze kwenye mahitaji ya nchi yanayohitajika hivi sasa kwani tayari baadhi ya fani ikiwemo Sheria mahitaji yake si makubwa hasa ikizingatiwa na wingi wa wahitimu wanaohitimu katika vyuo vikuu kila mwaka hapa nchini.Dk. Shein alisema kuwa akiwa Mkuu wa Chuo atatimiza wajibu wake ipasavyo na ataendelea kuwa karibu na Chuo sambamba na kufuatilia kwa karibu shughuli za Chuo hasa kutokana na dhama hiyo aliyopewa kwa mujibu wa sheria.“Pamoja na majukumu mengine niliyonayo lakini na hili ni langu na nitaendelea kulitekeleza kwa moyo wangu wote kwa kushirikiana na wale wote wanaohusika”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kugharamia masomo ya elimu ya juu na kila mwaka inajitahidi kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodhaminiwa na serikali kwa kadri hali inavyoruhusu. Dk. Shein alisisitiza kuwa hadi mwisho wa mwaka huu wa 2012 Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu inaowadhamini kutoka wanafunzi 209 wapya hadi 800 na kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar kutoka Tshs. Bilioni 4 hadi Bilioni 8.Kwa kutilia mkazo hatua hiyo, Dk. Shein aliitaka Bodi iendelee kuwa makini na kuhakikisha inafanya uadilifu katika uteuzi wa wanafunzi wanaostahiki kupewa mikopo”Bodi isipendee mtu kwa sura na haipendezi katika kuwasaidia wananchi wa nchi moja ukapitisha upendeleo.. tufuate utaratibu uliopo”,alisisitiza Dk. Shein.Aidha, Dk. Shein aliwataka na wale wanaopewa mikopo kuhakikisha kwamba fedha hizo walizokopeshwa wanazirudisha baada ya kumaliza masomo yao ili na wengine wanufaike nazo.Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuwajengea uwezo watu wake ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia vikundi vya ushirika vya vijana na wanwake na kusisitiza kuwa hivi karibuni Serikali itazindua mfuko kwa ajili ya kuvisaidia vikundi mbali mbali.