RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inagawa miche ya Mikarafuu iliyokomaa ili kuepuka uwezekano wa miche hiyo kufa muda mfupi baada ya kuoteshwa mashambani.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar katika mkutano wa Baraza la tatu la Biashara, ambao ulijadili maazimio yaliofikiwa katika Jukwaa la Tisa la Biashara lililofanyika mwezi Novemba 21, 2018, mkutano ukilenga kuifahamisha jamii juu ya makubaliano ya mambo muhimu ya mwenendo wa kibiashara yaliofikiwa kati ya sekta binafsi na Serikali.
Alisema ni muhimu kwa Wizara hiyo kuhakikisha miche ya Mikarafuu inayotolewa na serikali kwa ajili ya kugaiwa wakulima inafikia miaka miwili ili kuondokana malalamiko ya baadhi ya wakulima kuwa miche mingi hufa baada ya muda mfupi wa kupandikizwa, kwa vile haikuwa imekomaa.
Alisema ni muhimu kwa watendaji wanaoshughulikia ugawaji huo, kuhakikisha miche hiyo inawafikia walengwa wa kilimo hicho, ili kuondokana na manung’uniko ya baadhi ya wakulima kukosa miche hiyo.
Aidha, aliwataka wananchi, hususan kiiswani Pemba wenye taarifa za mashamba ya mikarafuu yenye mkanganyiko wa uhalali wake kutoa taarifa Serikalini ili yaweze kufuatiliwa na kutathminiwa.
Dk. Shein aliipongeza Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa kuanza kushughulikia maeneo ya kihistoria na mambo ya kale, hatua inayothitisha umuhimu wa Serikali kuanzisha Wizara hiyo.
Alisema kuna kazi kubwa na endelevu inayohitaji kufanywa ili kuimarisha sekta ya utalii nchini, kupitia maeneo ya kihistoria na mambo ya kale.
Alisema Zanzibar ina utajiri mkubwa wa vivutio vya Utalii, hivyo hatua ya Wizara hiyo kuanza kuviimarisha vivutio vya kihistoria vilivyopo ni ya kutia moyo.
Rais Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuwapatia mafunzo watendaji wa Wizara hiyo pamoja na kuitaka Jumuiya ya Uwekezaji sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) na Jumuiya ya watembeza Watalii Zanzibar (ZATO) kushirikiana na Serikali katika kufanikisha azma ya kuimarisha utalii nchini.
Alisema Wizara hiyo ina wajibu wa kushirkiana na taasisi mbali mbali za Serikali ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali katika sekta ya Utalii, ikiwemo changamoto ya ajira kwa vijana wa Zanzibar.
Akigusia, suala la mrundikano wa Makontena Banadarini, Dk. Shein alisema ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri ndio suluhisho la pekee katika kuondokana na mrundikano wa makontena Bandarini.
Alieleza kuwa idadi ya wananchi wa Zanzibar imeongezeka sambamba na harakati za kimaisha kuongezeka sana, wakati ambapo ukubwa na uwezo wa Bandari ya Malindi umebaki kama ulivyokuwa miaka mingi iliopita, hivyo kutokuendana na mahitaji halisi ya wakati uliopo.
Alisema kwa vipindi tofauti Serikali imelijadili suala hilo na kutokuwepo njia mbadala ya kulimaliza, hivyo akawataka wafanyabiashara kushirikiana na Serikali ili kujenga nguvu ya pamoja itakayofanikisha ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri.
Alisema hoja ya kuanzisha Bandari kavu kamwe haiwezi kufanyakazi kwa kuzingatia changamoto kadhaa ziliopo, ikiwemo uwezo mdogo wa barabara ambazo kimsingi haziwezi kuhimili mizigo mizito.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwataka wadau katika sekta binafsi kufanya juhudi kuimarisha sekta hiyo ili iweze kuchochea maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.
Alisema ni muhimu kwa sekta hiyo kushirikiana na serikali na kufanyakazi kwa mashirikiano ya karibu kwa kuelewa kuwa sekta zote hizo zinapaswa kujenga uchumi wa Taifa moja.
Alisema uchumi wa mataifa yote Duniani hutegemea mashirikiano ya pamoja kati ya sekta binafsi na Serikali.
Nae, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema ukodishwaji wa mashamba ya mikarafuu ya eka tatu za Serikali hufanyika kupitia Kamati maalum, ambapo ugavi wa fedha zinazopatikana hugawiwa kati ya Serikali na mhudumiaji, kutegemeana na mazingira ya shamba linavyoshughulikiwa na kuendelezwa.
Alisema , Serikali inaendelea na mchakato wa kuyaandalia hati miliki mashamba yote ambayo hadi sasa hayajatambuliwa, ili wananchi wanaoyatunza waweze kuyaendeleza kisheria.
Alieleza kuwa Serikali imekuwa na utaratibu wa kuyachukuwa mashamba hayo ya mikarafuu kwa kuwa na hati zake na kujiridhisha kuwa ni eka za Serikali .
Aidha, Waziri Habari,Utalii na Mambo ya Kale, Mahamoud Thabit Kombo alisema Wizara hiyo imeendelea na juhudi za kurejesha uhalisia wa maeneo mbali mbali ya Kihistoria, yaliopoteza haiba yake kutokana na sababu tofauti, kwa kuyafanyia ukarabati pamoja na kuyawekea ulinzi.
Alisema kupitia mpango maalum, Wizara hiyo imeanza kuyafanyia ukarabati maeneo ya kihistoriia na mambo ya Kale ya kwa Bihole, Makamandume, Fukuchani, Chwaka Tumbe pamoja na Mwinyimkuu.
Alisema kazi hiyo itaendelea kufanyika hatua kwa hatua kuambatana na upatikanaji wa fedha hadi kuyafikia maeneo yapatayo 100 ambayo ni vivutio vikubwa vya utalii hapa nchini.
Aliiomba Jumuiya ya watembeza watalii (ZATO) kuwaelimisha wadau wake wote umuhimu wa kuondokana na utamaduni wa kuwarubuni watendaji wa Wizara hiyo ili kukwepa ulipaji wa tozo kutoka kwa wageni.
Akigusia urejeshaji wa turathi za asili kutoka nchi mbali mbali Duniani, Waziri Kombo alisema mkataba wa mashirikiano uliotiwa saini mwezi Novemba 2018 kati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Oman umefungua majadiliano ya kurejeshwa vitu mbali mbali vyenye asili ya Zanzibar, ambavyo vilitoweka kwa sababu mbali mbali.
Alisema vitu hivyo vimeenea katika nchi mbali mbali Duniani, ikiwemo Oman na Ujerumani.
Nae, Mjumbe wa Bodi ya Baraza hilo Ali Amour, aliishauri Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kuwa na mpango maalum wa kupata fedha zitakazowezesha taasisi zinazosimamia matengenezo ya maeneo ya utalii kufanikisha jambo hilo, ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Vile vile, Mjumbe wa Baraza hilo, Naila Majid Jidawi, aliomba Serikali inapaswa kuangalia kwa kina changamoto za upatiokanaji wa ajira zinaowakabili vijana wa Zanzibar kupitia sekta ya Utalii, ikiwemo kufukuzwa kazi kiholela katika Mahoteli.
Nao, baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo, wakichangia mada juu ya jukumu la Wawekezaji kushirikiana na jamii katika sekta ya utalii ili kujenga uchumi wa jamii, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said alisema kuna umuhimu kwa Serikali pale inapofanya biashara kubwa kama vile ya uwekezaji wa mafuta na gesi ikahakikisha inalinda biashara za wananchi wake.
Akinasibisha kauli yake, Mwanasheria huyo alitoa mfano wa Uwekezaji katika sekta ya Utalii maeneo ya Kiwengwa na kusema kile kilichotarajiwa kuonekana katika maeneo hayo ni kwa wawekezaji kushirikiana na Serikali na kuleta matokeo chanya ya kuwepo huduma bora katika nyanja mbali mbali za kijamii, kama vile afya na elimu.
“Ili faida iweze kuonekana na wananchi waweze kunufaika kutokana na faida wanayopata wawekezaji…… , kwa uwekezaji huu tuna shule nzuri, kwa uwezekezaji huu tuna vituo vya afya bora”, alisema.
Mjumbe wa Baraza hilo Mohamed Bhaloo alisema ni muhimu kwa wananchi wakapewa fursa ya kuchagua aina ya mradi wanaohitaji katika maeneo yao badala ya Mwekezaji binafsi kuchaguwa aina ya mradi wa kusaidia.
“Mimi sioni kama mtu anaweza kuwekeza mradi wa Dola milioni kumi, halafu kutoa Dola laki moja iwe taabu”, alisema.
Akitoa mada inayoakisi umuhimu wa kulinda na kuendeleza uchumi wa Buluu (Blue Economy) kupitia sekta ya Utalii, Mkurugenzi Mtendaji wa Chambers of Commerce Hamad O. Hamad alisema ni muhimu kulinda maeneo ya visiwa vilivyoanishwa ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira, kuwepo matumizi mazuri ya rasilimali, pamoja na kupiga marufuku matumizi ya vyombo vya moto katika fukwe.