RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa sekta ya habari ni kichocheo kikubwa cha maisha ya mwanaadamu hivyo lazima habari ziandikwe kwa usahihi, kwa ukweli na kwa umahiri wake.Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa studio za kisasa za Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC -TV), zilizopo Kikwajuni Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa sekta ya habri ni kiungo muhimu katika kuwafahamisha wananchi hatua mbali mbali za maendeleo zinapigwa pamoja na kuwapa elimu na maarifa ya kuwasaidia katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.Alieleza kuwa hiyo ndio sababu ya Mwasisi wa Mapinduzi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kwa miaka ya awali ya Mapinduzi na kwa kutekeleza Sera za ASP, aliamua Zanzibar ianzishe kituo cha Televisheni sambamba na kuimarisha kituo cha redio cha Sauti ya Tanzania Zanzibar.
Alieleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zenye historia ndefu ya sekta ya habari kwa mfano uandishi na uchapaji wa magazeti ulianza mwaka 1875 hatua ambayo iliiwezesha Zanzibar kupata fursa ya kutumia mitambo ya upigaji chapa ya aina mbali mbali kwa awamu na katika maeneo tofauti.