RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameungana na mamia ya wananchi katika maziko ya mwanasiasa maarufu Issa Kassim Issa ‘Baharia’ yaliofanyika kijijini kwake Uroa, Wilaya ya Kati Unguja.Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariamu Mwinyi alikuwa miongoni mwa walioshiriki katika maziko hayo.

Wengine waliohudhuria maziko hayo ni pamoja Naibu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid Maulid, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Viongozi wa Dini, wanasiasa pamoja na viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali.

Aidha, katika maziko hayo, Rais Dk. Mwinyi alishiriki katika dua ya kumuombea maiti pamoja na sala iliofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Uroa na badae kufika nyumbani kwa wafiwa kwa ajili ya kutoa mkono wa pole.

Akisoma wasfu wa Marehemu Katibu wa Vijana (CCM) Mkoa wa Kusini Unguja Aboud Said Mpate alisema Marehemu Issa Kassim Issa alizaliwa mwaka 1957 katika Kijiji cha Uroa Wilaya kati Unguja na kupata elimu za msingi na Sekondari hadi Kidato cha Nne (F.IV) katika skuli ya Uroa na hatimae kupata mafunzo ‘Field Engineer Logistic Commmunication’  katika Jeshi la wananchi wa Tanzania.

Alisema wakati wa uhai wake Marehemu alijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977 na kufanikiwa kushika nyadhifa mbali mbali za Uongozi ndani ya chama hicho, ikiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mbunge wa Jimbo la Mpendae (2005-2010) pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa Kusini Unguja Unguja mwaka 2017, wadhifa aliodumu nao hadi anafikwa na mauti.

Kufuatia kifo hicho Chama cha Mapinduzi Mkoa Kusini Unguja kimetoa mkono wa pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa na wanachama wa CCM na Jumuiya zake na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba, sambamba na kumuomba Mwenyezi Mungu kuiweka roho ya Marehemu mahala pema peponi.

Marehemu Issa Kassim Issa aliefariki jana katika Hospitali ya Rufaa Muhimbili Jijini Dar es Salaam ameacha vizuka wawili , watoto 12 na wajukuu saba