Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi jana aliwaongoza Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na viongozi na wafanyakazi wa “VIGOR A TURKY’S GROUP OF COMPANIES”, katika Maulidi ya kuadhimisha Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Makampuni hayo na kufanyika huko katika viwanja vya kiwanda cha Zainab Bottles, Mombasa Mjini Zanzibar.
Sherehe hizo za Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanywa na “VIGOR A TURKY’S GROUP OF COMPANIES”, kila mwaka pia, zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini na Serikali akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih.
Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa “VIGOR A TURKY’S GROUP OF COMPANIES”, Sherehe hizo za Maulid zilizanzishwa na Marehemu Salim Hassan Turky ambaye ndiye aliyekuwa muasisi wa Maulid hayo ambaye pia, alikuwa Mwenyekiti wa “VIGOR A TURKY’S GROUP OF COMPANIES”,
Mbali ya Maulid hayo pamoja na nasaha zilizotolewa juu ya umuhimu wa kumsalia Mtume Muhammad (S.A.W) sambamba na kufuata nyayo zake, hadhara iliyokuwepo katika Maulid hayo pia, ilitumia fursa hiyo kumuombea dua Muasisi wa Maulid hayo Marehemu Salim Hassan Turky, ndugu, jamaa, viongozi pamoja na Waislamu wote, dua iliyoongozwa na Sheikh Maalim Ali Hamed Jabir.
Pamoja na hayo, uongozi wa Makampuni hayo hiyo chini ya Mwenyekiti wake Taufiq Turky uliahidi kuyaendeleza yale mema yote yaliyoachwa na Muasisi huyo huku akimuhakikishia Alhaj Dk. Mwinyi kwamba “VIGOR A TURKY’S GROUP OF COMPANIES”, itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sanjari na kuziunga mkono juhudi za Rais Dk. Mwinyi za kuwaletea maendeleo Wazanzibari wote.