RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza mazishi ya Mweyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Amani Kichama marehemu Juma Khamis Haji (Juma Resi), yaliyofanyika kijijini kwao Upenja, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali, pamoja na wananchi, ndugu na jamaa walihudhuria katika mazishi hayo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdallah Juma Mabodi pamoja na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali.Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Juma Resi katika Msikiti wa Upenja, Wilaya ya Kaskazinii ‘B’, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika uhai wake Marehemu Juma Khamis Haji (Juma Resi), aliyezaliwa mwaka 1951 amekitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa Diwani wa Jimbo la Muembemakumbi, Katibu wa Jimbo la Muwembemakubi, Mwalimu wa Madarasa ya Itikadi pamoja na makundi ya Vijana wa Hamasa.
Nafasi nyengine ni Afisa Uhamasishaji Wilaya, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa, Katibu Mwenezi Wilaya ya Mjini, Katibu Mwenezi Wilaya ya Amani, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Kichama, cheo ambacho alikitumikia mpaka mauti yalipomfika.
Wakati huo huo, mara baada ya mazishi, Alhaj Dk. Shein alikutana na familia ya marehemu Juma Resi hapo hapo kijijini kwao Upenja na kutoa mkono wa pole kwa familia na wafiwa wote pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akisisitiza kuendelea kumuombea dua marehemu.
Marehemu Juja Resi ameacha vizuka wawili pamoja na watoto kumi na mbili (12) na Wajukuu 23, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya maremu mahala pema peponi, Amin.