CHUO Kikuu Huria cha Tanzania kimetakiwa kuangalia mitaala yake jinsi itakavyosaidia kuandaa Wataalamu watakaoweza kutekeleza dhamira ya kujenga uchumi mpya unaozingatia matumizi ya rasilimali za bahari au uchumi wa Buluu ambao ni ajenda maalum ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane.Rai hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika Mahafali ya 40 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika uwanja wa Mao Ze Dong, Zanzibar ikiwa ni Mahafali ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar tokea kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho mnamo mwaka 1992.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alikihimiza Chuo Kikuu hicho ambacho Mkuu wake ni Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda, kufanya tafiti zenye lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii katika nyanja zote za maendeleo.Alisema kuwa kufanya tafiti ni moja ya majukumu ya msingi ya Vyuo Vikuu na matokeo ya utafiti yawafikie watu na yawe na manufaa kwao.
Akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alitoa rai kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuangalia maeneo ya ushirikiano kati yake na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).Aliyataja maeneo ya ushirikiano katika masuala mbali mbali hasa utafiti,Tehama, mbinu za kisasa za ufundishaji na kutafuta fursa za ajira nje ya nchi kwa wahitimu wa shahada za lugha ya Kiswahili zinazotolewa na vyuo hivyo.Alikitaka chuo hicho kutumia changamoto walizonazo kua ni futsa na wala zisiwakatishe tamaa katika kufikia Dira na Malengo ya kuanzishwa kwa Chuo hicho.
Alisema kuwa kufanyika kwa mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar sio tu kuna umuhimu wa kihistoria kwa chuo hicho bali pia, ni hatua muhimu katika kuimarisha Muungano wa Tanzania kwa dhamira ile ile ya waasisi wa Taifa hili Hayati baba wa Taifa Mwalimu Juliaus Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.Aliongeza kuwa hiyo ni fursa nyengine ya kuimarisha na kuendeleza umoja wa Watazania baada ya chuo hicho kuanzisha Matawi yake hapa Unguja mwaka 1995 na kule Pemba mwaka 2004, na kupongeza kazi nzuri ya chuo hicho tokea kuanzishwa kwake ambapo wanafunzi wapatao 4,534 wamedahiliwa kutoka Zanzibar katika programu na ngazi mbali mbali.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kati yao wapo waliohitimu na walisema kuwa wapo viongozi mbali mbali wa Serikali ambao ni matunda ya Chuo hicho na kupongeza kazi nzuri inayofanwya na chuo hicho.Alikipongeza Chuo hicho kwa kufikia malengo ya kuanzishwa kwake ambapo alisema kuwa Chuo hicho kina rekodi nzuri katika Afrika kwa kushika nafasi ya kwanza na cha 16 kati ya Vyuo Vikuu Huria 159 duniani na cha 6 kwa ubora miongoni mwa Vyuo Vikuu 54 vya Tanzania
Pia, alitumia fursa hiyo kwa kuwapongeza wahitimu wote kwani anatambua kwamba hatua hiyo haikuwa rahisi bali ni matokea ya jitihada kubwa waliyofanya hadi kuhitimu kwao na kusema kwamba jamii ina mategemeo makubwa kwao.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Chuo hicho kimekuwa kikiwafikia Watanzania kila kona sambamba na kuwafikia wananfunzi hata walio nje ya Tanzania.
Aidha, alitoa ahadi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinathamani sana michango ya chuo hicho na zitaendelea kukipa kila aina ya ushirikiano ili kukiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa elimu ya juu ina umuhimu mkubwa wa maendeleo ya nchi kwani hatua hiyo ndiyo inayowajenga vijana na kupatiwa ujuzi muhimu wa kutumikia maendeleo ya nchi.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Chuo hicho ni Chuo pekee miongoni mwa vyuo vikuu vya Tanzania kilichoweza kuendelea kutoa huduma za kufundisha na jitahidini kupitia mtandao bila ya kuathirika na janga la UVIKO 19.Alieleza umuhimu wa kubuni programu na kozi mbali mbali ili chuo hicho kiendelee kuwa chemchem ya Wataalamu mahiri wenye uwezo wa kushindana katika soko la ndani na la Kimataifa.
Alisisitiza haja ya ya kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya kupata wataalamu watakaokidhi katika utekelezaji na mipango mikuu ya maendeleo ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa Tanzania wa 2025 (Vision 2025), Dira ya Maendeleo ya Zanzibar (2050) pamoja na mipango mengine ya kikanda na Kimataifa.
Akitoa maelezo yake, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omar Juma Kipanga alieleza mikakati ya Serikali katika kukiimarisha Chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuviimarisha vituo vitano hapa nchini kikiwemo kituo cha Pemba.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said kwa upande wake alisisitiza haja ya kuendelezwa kwa mashirikiano kati ya pande mbili hizi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili maendeleo na mafanikio zaidi yaweze kupatikana.
Nao viongozi wakuu wa Chuo hicho walieleza mafanikio waliyoyapata katika chuo hicho pamoja na changamoto zilizopo.
Jumla ya wanafunzi 30, wamehitimu Shahada za Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa kati ya wahitimu wote 3,110 waliohitimu mwaka huu katika programu na ngazi mbali mbali za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wakiwepo pia wanafunzi waliohitimu kupitia Chuo hicho walioko katika Chuo Kikuu Huria cha Laweh cha nchini Ghana.