Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi na kusisitiza haja ya kwenda kuzitangaza fusra za kujenga uchumi wa nchi ikiwemo Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar.

Mabalozi ambao alikutana nao leo Rais Dk. Mwinyi Ikulu Zanzibar na kufanya nao mazungumzo ni Balozi Anisa Mbega anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini India, Balozi Togolani Edriss Mavura anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Korea Kusini na Balozi Innocent Shiyo anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba nchi kama Korea Kusini imepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika kuitumia bahari kama sehemu moja wapo ya kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuwa na viwanda vingi vya uvuvi, bandari na viwanda vya meli hatua ambayo inaweza kusaidia katika kuendeleza Sera ya Uchumi wa Buluu kwa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mabalozi hao kwenda kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na vivutio vyake kadhaa vilivyopo hasa kwa nchi za Korea Kusini na India ambako bado watalii wake wanaokuja kuitembelea Zanzibar hawajawa wengi.

Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wake kupitia ujenzi wa bandari ya kisasa ambayo itajumuisha shughuli mbali mbali ambapo pia, itahitaji wawekezaji.

Alieleza mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha inaijengea uwezo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) iweze kufanya kazi ipasavyo na kuwa kituo maalum kitakachotoa huduma zote za uwekezaji kwa muda mfupi sambamba.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mabalozi hao kusaidia kutafuta soko kwa ajili ya zao la mwani kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo sanjari na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuja kuekeza katika sekta ya viwanda pamoja na gesi asilia hapa Zanzibar.

Nao Mabalozi hao kwa upande wao walimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa juhudi za makusudi watazichukua katika kuhakikisha wanatekeleza vyema majukumu waliyopewa na kutumia fursa hiyo kutoa shukurani zao kwa Rais kutokana na maelekezo aliyowapa.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu na kueleza haja kati ya Zanzibar na Kenya kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo hasa katika sekta ya biashara na uwekezaji.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao kwa pamoja walisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuimarisha sekta hizo hasa ikizingatiwa kwamba pande mbili hizo zina uhusiano mwema pamoja na kuwepo vyanzo ya mashirikiano katika sekta hizo za uchumi.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kurasimishwa kwa biashara na kuwekewa mazingira mazuri ya bandari na vyombo vya usafiri kwa wafanya biashara wa pande mbili hizo ili kuweza kufanya biashara zao vizuri hasa ikizingatiwa ukaribu uliopo baina ya Zanzibar na Kenya.

Viongozi hao pia, walieleza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kihistoria wa utamaduni uliopo baina ya Kenya na Zanzibar ambao unahitaji kuendelezwa na kuimarishwa zaidi ili uweze kuleta manufaa kwa pande mbili hizo