RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ofisi za Zanzibar, Laxm Bhawani kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Ofisi hiyo na akamhakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kumuunga mkono ili kufikia mafanikio katika maeneo anayofanyia kazi.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Jijini hapa, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Ofisi za Zanzibar Laxmi Bhawani.

Alisema Ofisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuhakikisha huduma mbali mbali ikiwemo za Afya na Elimu zinaimarika hapa nchini, sambamba na kuondokana na umasikini pamoja na utapia mlo kwa watoto.

Alisema upatikaji wa lishe kwa watoto ni jambo muhimu na akabainisha kazi kubwa inayopaswa kufanyika kufanikisha jambo hilo, kwa kuzingatia takwimu zilizopo za watoto wenye utapia mlo.


Alisema katika kuimarisha huduma za Afya, Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika uwekaji wa miundo mbinu katika sekta hiyo pamoja na kuwajengea uwezo watendaji wake.


Dk. Mwinyi, alitolea mfano wa dhamira ya Serikali ya kujenga Hospitali katika Wilaya zote Unguja na Pemba na hivyo kuwepo mahitaji makubwa ya wafanyakazi wa huduma za Afya katika nyanja mbali mbali.

Rais Dk. Mwinyi, alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, imekuwa ikifanya juhudi kuona kwa namna gani itaweza kuimarisha kiwango cha elimu hapa nchini kupitia sera ya elimu iliopo.
 
Mapema, Kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, Ofisi ya Zanzibar Laxmi Bhawani, alimueleza Rais Dk. Mwinyi masuala mbali mbali yanayotekelezwa na Ofisi yake, ikiwemo ya kufanikisha Programu ya Ulimwengu ya kuwarejesha watoto shule, mitaala ya walimu ya kuinua viwango vya ufundishaji, sambamba na   hatua ya kushirikiana na taasisi mbali mbali, ikiwemo Mradi w akunusuru Kaya maskini (TASAF)  katika kufanikisha mpango wa kupunguza umasikini nchini.