RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongezwa na Wajumbe wa Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake tokea aingie madarakani.
Akitoa pongezi hizo kwa kuungana pamoja na Wajumbe hao, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kabla ya kuanza kwa mkutano wa Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, uliofanyika Ikulu ya Chamwino Dodoma alitoa pongezi hizo kwa Rais Dk. Mwinyi pamoja na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliipongeza hotuba aliyoisoma Rais Dk. Mwinyi hapo jana (Novemba 07,2021) na kusema kwamba ni hotuba iliyosheheni mafanikio.
“Ahadi yetu kwenu tutaendelea kuwaunga mkono ili tuweze kukamilisha yale ambayo wananchi wanatarajia tuwatimizie, hongera sana nasi tutawaunga mkono kikamilifu na Mungu awabariki awape nguvu na afya muendelee kuwatumikia wananchi”,alisema Rais Samia.
Wajumbe hao wa Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walionesha furaha kubwa kwa Rais Dk. Mwinyi kufuatia pongezi hizo sambamba na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka mmoja wa uongozi wake.
Wakati huo huo, viongozi wakuu wa CCM, waliungana pamoja katika hafla maalum ya chakula kilichoandaliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa Makatibu wa CCM wa Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania.
Mapema akiondoka Zanzibar kuelekea Mji Mkuu wa Tanzania, Dodoma, Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi alipewa zawadi mbali mbali na Uongozi na wafanyakazi wa Kampuni ya ‘Tropical Air’ kufuatia kutimiza mwaka mmoja tokea aingie madarani.