Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kurejea kwa safari za anga za moja kwa moja kutoka Ufaransa hadi Zanzibar kupitia Shirika la Ndege la Air France kutatoa msukumo mkubwa katika sekta ya Utalii na kukuza uchumi wa Taifa.Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hijilaoui, aliefika kujitambulisha na kupata fursa ya kuzungumzia miradi mbali mbali, ambapo nchi hiyo itaisaidia Zanzibar.
Amesema kurejea kwa safari za mashirika kadhaa ya Ndege Duniani kumeifanya Zanzibar kupokea idadi kubwa ya Watalii , na hivyo kuisaidia kuimarisha sekta ya Utalii ambayo imeathirika kutokana na janga la Uviko.Dk. Mwinyi alisema Zanzibar inahitaji Kampuni mbali mbali zenye azma ya kuwekeza katika sekta nishati ya Umeme, ikiwemo wa jua ili kuongeza uwezo wake wa kusambaza nishati hiyo kwa wananchi.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na tatizo la upungufu wa huduma za maji safi na salama, hususan katika maeneo ya hoteli za kitalii, hivyo misaada ya nchi katika sekta ya maji ni jambo la muhimu.Dk. Mwinyi aliipongeza Ufaransa kwa ushiriki wake wa kusaidia miradi mbali mbali ya kijamii na maendeleo na kubainisha hatua hiyo itafanikisha na kuharakisha azma ya Zanzibar kukuza uchumi wake kupitia Uchumi wa Bluu.
Alimueleza Balozi huyo maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Mafuta Mangapwani, inayohusisha banadari tofauti na kubainisha fursa kadhaa za uwekezaji zilizopo, hivyo akatoa wito kwa Wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuwekeza.Alisema azma ya Serikali ya kuanzisha kikosi maaalum cha ulinzi wa watalii (Tourism Police) ni kuhakikisha Watalii wote wanaofika nchini wanakuwa salama katika muda wote wawapo nchini.
Mapema, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajilaoui aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uhusiano na ushirikiano wake na Ufaransa, huku akipongeza uwepo wa amani na utulivu nchini, sambamba na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake.Balozi Nabil aliahidi kuwashajihisha Wawekezaji kutoka Ufaransa kuja nchini kuwekeza katika miradi mbali mbali ya Maendeleo.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amekutana na ujumbe wa Madaktari kutoka ‘Hackland University Hospital’ ya nchini Norway, ambao wamekuwa wakisaidia Hospital ya Wagonjwa wa Akili Kidongochekundu katika nyanja za miundombinu, vifaa pamoja na mafunzo na hivyo akatumia fursa hiyo kuomba kupanua wigo wa misaada yao.