MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM, ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alikuwa miongoni mwa Viongozi wakuu wa Chama cha Mapinduzi walioshiriki katika Semina kuhusu Sensa ya Watu na makaazi ya mwaka 2022,Semina hiyo ikiwa sehemu ya Kikao cha kawaida cha Halmashauri kuu ya CCM Taifa, kilifanyika katika Ukumbi wa ‘Jakaya Kikwete Conversion Centre’ chini ya Mwenyekiti wa CCM Mama Samia Suluhu Hassan.
Akitoa majumuisho ya semina hiyo, Mama Samia alisema kukamilika vyema kwa sensa hiyo kuitaiwezesha Serikali kuibuwa miradi kadhaa itakayohitaji kutekelezwa katika maeneo tofauti, kwa kigezo kuwa teknolojia inayotumika (satellite) kufanikisha sensa hiyo ina uwezo wa kubaini mambo mengi yakiwemo ya kiusalama.
Alisema Serikali imeajiandaa kikamilifu kwa fedha na watalamu wa kufanikisha sensa hiyo, hivyo akatumia fursa hiyo kuwashukuru Makamisaa, Makamishna na wanakamati kwa kufanikisha hatua ya kwanza ya sensa ya majaribio, sambamba na kuwataka kuendeleza vyema jukumu lilioko mbele yao, huku wakitambua kuwa serikali iko nyuma yao.
Aidha, aliwataka wajumbe hao kuondokana na utamaduni wa ‘kuwazonga’ wasimamizi wa sensa hiyo kuhusiana na suala la kuwapatia ajira vijana wao, kwa kigezo kuwa sensa ya mwaka 2022 inahitaji watumishi wenye sifa maalum.
Nae, Makamo wa Rais wa Jmauhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango alisema miongoni mwa faida kubwa zitakazopatikana kutokana na kufanyika kwa sensa hiyo ni kuweza kujua mgawanyo wa Huduuma za Fedha hapa nchini.
Mapema, Kamisaa wa Sensa 2022, Anna Makinda alisema matayarisho kwa ajili ha Sensa hiyo yamefikia asilimia 65 baada ya kukamilika sensa ya majaribio iliyofanyika mwezi Augosti 2021 katika Mikoa 18 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar.
Alisema sensa hiyo itajikita katika matumizi ya TEHAMA, kuanzia ngazi za Vitongoji na kuhusisha dodoso za jamii, majengo pamoja na anwani za makaazi ambapo tayari hatua hiyo imekamilika kwa asilimia mia moja.
Alieleza kuwa kazi kubwa iliopo mbele ya taasisi zinazosimamia sense hiyo ni kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kushiriki sensa, na kusema nguvu ya pamoja inahitajika kufanikisha jambo hilo.
Akigusia suala la maandalizi kwa makarani na wasimamizi wa sensa ya 2022, alisema watendaji hao watatoka katika maeneo wanayoishi, huku mkazo ukiwekwa katika kuwapata vijana wenye elimu ya sekondari.
Aidha, Kamisaa wa Sensa Balozi Mohamed Hamza alisema sensa hiyo itazisaidia serikali zote mbili kupanua wigo katika ukusanyaji wa mapato, sambamba na kuandaa mipango ya maendeeo katika maeneo yote, kuanzia ngazi za Vitongoji.
Aliwaomba wajumbe wa NEC kuunga mkono juhudi za serikali zote mbili pamoja na kusaidia kufanikisha kazi ya kuielimisha umma katika maeneo walioko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa sensa mwaka 2022 (ambae pia ni Mtakwimu mkuu wa Serikali) Dk. Albina Chuwa alisema Serikali inalazimika kufanya sensa mwaka 2022 ili kukidhi mahitaji ya kitaifa, kimataifa na kikanda na akabainisha utofauti uliopo kati ya sensa ya 2022 na zile zilizopita.
Alieleza kuwa Sensa ya 2022 imepanua wigo wa madododso, hatua inayotokana na mahitaji ya mipango ya Takwimu Duniani kupanuka na kusema itahusisha masuala 120 wakati sensa ya mwisho iliyofanyika ilihusisha masuala 64.
Alisema pamoja na mambo mengine sensa hiyo itasaidia katika kufanya tathmin ya Dira ya Mipango ya Maendeleo kwa serikali zote mbili.
Alisema miongoni mwa faida kubwa zitakazotokana na sensa hiyo ni pamoja na kubainisha mahitaji halisi katika sekta za elimu, afya na maji na nyenginezo.
Alisema kwa upande wa siasa, matokeo ya sensa hiyo yatabainisha eneo la uchaguzi na kubaini wingi wa wapiga kura sambamba na mikakati ya ushindi kwa chama cha Mapinduzi.
“ Takwimu hizo zitapatikana ngazi za Serikali za Mitaa na tukumbuke kuwa mwaka 2024 ndio uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika”, alisema.
Katika hatua nyengine Mtaalmu wa Teknolojia Benedict Mgambi alifafanua kuwa kwa mara ya kwanza Taifa litaweza kupata idadi halisi ya majengo yaliopo nchini, sifa zake pamoja na yale yanayofanyika katika majengo hayo, jambo ambalo Jeshi la Polisi , TRA na mamlaka nyengine zitaweza kuzifanyia katzi taarifa hizo.
Alisema takwimu hizo zitaoa taarifa za ulinganisho wa huduma za kijamii pamoja na teknolojia kubainisha utengaji wa maeneo mbali mbali ya Kijiografia, ikiwemo uoto wa asili, ardhi isiyo na mimea na aina ya kilimo kinachofaa katika sehemu husika.
Katika semina hiyo wajumbe walipata fursa ya kuishauri Serikali mambo mbali mbali ili kufanikisha sensa hiyo, huku wakielezea baadhi ya changamoto iliobuka katika sense iliopita m kwa ya baadhi ya wananchi kukwamisha zoezi hilo kwa sababu za kidini na kisisa, huku Mikoa mbali mbali ya kisiwani Pemba, Morogoro na Tandahimba, ikitajwa kukumbwa na kadhia hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambi rambi kwa kifo cha mwanasiasa mashuhuri hapa Zanzibar Issa Kassim Issa “Baharia” kilichotokea leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu zake , Dk. Mwinyi amewataka wafiwa wa marehemu kuwa na subira katika kipindi kigumu cha msiba wa ndugu yao,sambamba n a kumtakia maghufira kwa Mwenyezi Mungu marehemu huyo pamoja na kushiriki katika mapokezi .
Wakati wa jioni Dk. Mwinyi alishiriki katika mapokezi ya mwili wa marehemu Bandarini Malindi, Jijini Zanzibar.
Maziko ya Marehemu Issa Kassimu Issa yanatajiwa kufanyika kesho kijiji kwake Chwaka, Wilaya Kati Unguja