Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, leo Oktoba 30, 2021 amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni kumsaidia katika majukumu ya uendeshaji shughuli mbalimbali za Serikali.

Walioapishwa na Mhe. Rais hii leo ni pamoja na Mhe. Jaji Muumin Khamis Kombo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar. Awali Jaji Muumini alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Zanzibar. Naye Bi. Salma Ali Hassan Khamis ameapishwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka, Zanzibar. Awali Bi. Salma Ali Hassan Khamis alikuwa Mratibu wa mradi wa Uwezeshaji Kisheria na Upatikanaji wa Haki kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP).

Mhe. Rais Dk. Mwinyi pia amemuapisha Bi. Mwanamkaa Abdulrahman Mohammed kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Zanzibar. Awali, Bi. Mwanamkaa alikuwa Mwanasheria wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar.

Wakizungumza mara baada ya hafla hiyo, watendaji hao wameahidi kushirikiana na watendaji wengine wa Mahakama katika kuharakisha usikilizaji wa kesi ili wananchi waweze kupata haki zao kwa mujibu wa sheria. Aidha, wameeleza kuwa, watashirikiana na Jamii, Asasi zisizo za Kiserikali na zile za Kiserikali ili kuhakikisha kuna kuwepo na mikakati na mifumo bora katika mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto.