Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amewahakikishia mazingira mazuri ya kufanya Uwekezaji Visiwani Zanzibar kwa wawekezaji wote wa ndani ambao wangependa kuja kuwekeza Zanzibar.

Rais. Dk Mwinyi ameeleza hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Jumuiya ya Vyama vya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wake na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Bw. Masha Mshomba.

Aidha, Mhe. Rais amesema Zanzibar bado ina Fursa nyingi za Uwekezaji kwa Wawekezaji wa ndani ambao wangependa kuja kuwekeza visiwani Zanzibar katika maeneo mbali mbali na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo tayari kuweka dhamana katika miradi mikubwa ya maendeleo na yenye kuleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hizo za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Bw. Masha Mshomba amemweleza Mhe. Rais kuwa Mifuko hiyo iko tayari kuwekeza Zanzibar na wanafurahishwa na kuridhishwa na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dk. Mwinyi inavyofanya jitihada mbalimbali za kuvutia na kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.