RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein anaondoka nchini leo kuelekea Ras Al Khaimah katika Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kwa ziara ya wiki moja kufuatia muwaliko wa kiongozi wa nchi hiyo Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi.
Ziara hiyo ya Rais Dk. Shein huko Ras Al Khaimah inatarajiwa kuanza kesho tarehe 23 na kumaliza tarehe 28 Septemba mwaka huu 2019 ambapo katika ziara hiyo pia, atapata fursa ya kuzungumza na mwenyeji wake Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi.
Dk. Shein akiwa Ras Al Khaimah atakutana na uongozi wa Kampuni mbali mbali za nchi hiyo ikiwemo Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Ras Al Khaimah “Rak Gas”, Kampuni ya RAKEZ, Kampuni ya Mji wa Bahari wa Ras Al Khaiman, Mamlaka ya Uendelezaji Utalii ya Ras Al Khaimah, Mji wa Kisiwa cha Marjani pamoja na kukutana na Kampuni nyengine za mji huo ambayo yatapata fursa kueleza shughuli wanazozifanya.
Rais Dk. Shein akiwa Ras Al Khaimah atatembelea maeneo ya mji wa Ras Al Khaiman ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya kitalii katika mji huo na eneo la Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Rasyale ya maendeleo.
Aidha, Dk. Shein atakwenda Abu Dhabi kwa ajili ya kushuhudia utiaji wa saini Mkataba wa Mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Abu Dhabi kupitia Mfuko wa ‘Khalifa Fund’ wenye makao makuu yake nchini humo.
Rais Dk. Shein pia, ataungana na waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Sheikh Zayed uliopo mjini Abu Dhabi ambao ni msikiti maarufu duniani.
Katika ziara hiyo, Dk. Shein amefuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu, Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said, Balozi Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upande wa Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kurejea nchini Jumamosi ya tarehe 29 Septemba, 2019.
Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Rais Dk. Shein aliagwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na viongozi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama ambao waliongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.