Katika safari hiyo ya wiki moja Dk. Shein amefuatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein pamoja na Viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri wa Kilimo na Maliasili Mhe.Suleiman Othman Nyanga, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdillah Jihad Hassan.Viongozi wengine ni Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mhe.Haroun Ali Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe.Mahadhi Juma Maalim, Mshauri wa Rais, Ushirikiano wa Kimataifa na Uwekezaji Balozi Ramia Abdiwawa pamoja na Maafisa wengine wa Serikali.
Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tan Sang, Pia, atazungumza na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.Aidha, Dk. Shein atazugumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na wawekezaji wa nchi hiyo. Dk. Shein kabla ya kufanya mazungumzo hayo mapema anatarajiwa kuanza kuweka shada la maua katika makaburi ya mashujaa na kisha ataelekea katika jumba la Rais wa nchi hiyo kwa makaribisho rasmi.Pamoja na hayo, Dk. Shein anatarajiwa kufanya mazungumzo na vyombo vya habari ambayo yatafanyika mara baada ya Mhe. Dk. Shein kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa nchi hiyo.Pamoja na hayo, Dk. Shein atatembelea shughuli mbali mbali za maendeleo katika nchi hiyo yakiwemo maeneo ya kilimo, uvuvi, ufugaji pamoja na kuangalia shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi.