Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza ujio pamoja na azma ya Muigizaji Nyota wa Filamu za Kihindi, Sanjay Dutt ya kutaka kuekeza sambamba na kuwa Balozi wa kuitangaza Zanzibar kiutalii.Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Muigizaji Nyota huyo wa Filamu za Kihindi, Sanjay Dutt ambaye amekuja kuitembelea Zanzibar na kueleza jinsi alivyovutika na vivutio mbali mbali vilivyo Unguja na Pemba.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi pia, alimpongeza Nyota huyo kwa kueleza lengo lake la kuanzisha Kampuni yake hapa Zanzibar ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha tasnia ya Filamu hapa nchini sambamba na kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii Kimataifa.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba azma ya nguli huyo ya kuekeza Zanzibar katika sekta za maendeleo zikiwemo afya, elimu na nyenginezo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililowekwa na Serikali ya Awamu ya Nane la kuwarahisishia wananchi kupata huduma muhimu za kijamii hasa afya ambapo gharama kubwa zimekwua zikitumika hivi sasa kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi ikiwemo India, hivyo iwapo ataekeza katika sekta hiyo hapa nchini hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi amekuhakikishia nguli huyo wa filamu nchini India kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itampa kila ushirikiano katika kuhakikisha azma yake hiyo inafanikiwa na mipango yote aliyoipanga kwa Zanzibar inakwenda sawia.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Nyota huyo jinsi Serikali ya Awamu ya Nane ilivyodhamiria kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa ni sehemu maalum ya uwekezaji na jinsi ilivyoweka mikakati ya kuhakikisha hilo linatekelezwa baada ya Nyota huyo kueleza jinsi alivyovutiwa na mazingira ya kisiwa hicho cha Pemba.Rais Dk. Mwinyi alimueleza mchezaji huyo kuwa ujio wake una umuhimu mkubwa katika kuutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na vivutio vilivyopo huku akitumia fursa hiyo kumueleza nyota huyo Dira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa ambayo ni Uchumi wa Buluu na jinsi inavyokwenda sambamba na sekta ya utalii.
Nae Muigizaji Nyota wa Filamu za Kihindi Sanjay Dutt alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma yake ya kutaka kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo utalii, afya, miundombinu, sanaa na filamu pamoja na kutoa huduma kwa Jamii hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu.Sanjay Dutt ambaye amefuatana na Wasaidizi wake pamoja na uongozi wa Kampuni ya AFRICAB chini ya Mwenyekiti wake Yusuf Ezzi alianza kwa kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake huku akieleza azma yake ya kutaka kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo sanjari na kuwa Balozi wa kuitangaza Zanzibar.
Nyota huyo wa Filamu nchini India pia, alieleza azma yake ya kuanzisha Kampuni ya Filamu hapa Zanzibar sambamba na kuifanya Zanzibar kuwa ni sehemu moja wapo ya kuigiza Filamu zake kupitia Kampuni hiyo.Aliongeza kuwa amevutiwa na visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na uwepo wa vivutio vya kitalii ukiwemo mji Mkongwe huku akieleza ushabihiano uliopo kati ya visiwa vya Zanzibar na visiwa cha Bahamas ambavyo vimekuwa ni kivutio kikubwa cha wawekezaji na utalii kutoka sehemu tofauti za duniani wakiwemo wasanii.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yake na Rais wa Zanzibar, nguli huyo wa filamu kutoka nchini India alieleza azma yake ya kusaidia Jamii hapa nchini pamoja na kiu yake ya kuekeza Zanzibar huku akisisitiza utayari wake wa kuwa Balozi wa kuitanga Zanzibar.
Nae Waziri Utalii na Mambo ya Kale, Leila Muhamed Mussa akijibu masuala ya Waandishi wa habari alieleza jinsi Wizara yake ilivyovutika na utayari wa nyota huyo wa kuitangaza Zanzibar hasa ikizingatiwa hivi sasa Zanzibar inajikita kutafuta soko la utalii katika Bara la Asia.
Sanjay Dutt ambaye ni muigizaji nguli wa Filamu za Bollywood, ameigiza zaidi ya filamu 80 ukiachilia mbali zile alizoalikwa ambapo alionekana kwenye ulimwengu wa filamu kupitia filamu yake ya ‘Rocky’ ambayo iliongozwa na marehemu baba yake Sunil Dutt mnamo mwaka 1981.