RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha inavipatia maji safi na salama Vitongoji sita vilivyomo katika Shehiya za Muungoni na Kitogani sio zaidi ya Julai 30, 2021.Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo leo wakati alipokitembelea kituo cha maji kiliopo Kitogani, ambapo pamoja na ammabo mengine alitaka kufahamu changamoto zinazoawakabili wananchi wa maeneo hayo, ikiwa mwazno wa ziara yake ya kuutembeela Mkoa Kusini Unguja.
Amewataka watendaji wa Mamlaka hiyo kukamilisha mchakato wa kuvipatia huduma hiyo viongozi hivyo mapema iwezekanavyo kwa kukiwekea kituo hicho mundombinu kutoka Mradi wa Ras el Hemma wenye uwezo wa kuzalisha lita Milioni moja ya maji kwa siku, sambamba na kukiwekea kituo hicho Paipu mpya ili kiweze kutoa huduma kwa ukamilifu.
Aliwataka Viongozi wa ZAWA kuwajibika na kuwawajibisha watendaji wote wanaoshindwa kutekeleza majukumju yao ipasavyo, akibainisha kuwepo utendaji dhaifu wa watendaji katika mamlaka hiyo kwa kipindi kirefu.
Aliuagiza uongozi wa ZAWA kuhakikisha maeneo yote yanayomilikiwa na mamlaka hiyo, ikiwemo vituo vya maji yanapimwa na kupatiwa hati za umiliki.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema serikali itayafanyia matenegenzo majengo yote ya Skuli, ili kuona kunakuwepo mazingira bora ya upatikanaji wa elimu nchin i.
Akitembelea Skuli ya Sekondari Mtule, Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha ufaulu unaongezeka maskulini, hususan katika Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo taarifa zinabainisha kuwepo katika orodha ya skuli zinazofanya vibaya zaidi kitaifa.
Alitaka kuwepo mikakati maalum kuinua hali ya kielimu Mkoani humo, huku akiwataka wazazi kuunga mkono juhudi hizo.
Vile vile Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwatembelea Wajasiriamali wa Wilaya Kusini wanaozalisha bidhaa mbali mbali, hafla iliofanyika katika kiwanja cha mpira Paje na kuwataka Wakilishi wa Majimbo ya Wilaya hiyo kukaa pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, kuona namna gani ya kuwasaidia wajasiriamali hao katika kuwapatia mafunzo pamoja na masoko ya kuuzia bidhaa zao.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alitembelea Chuo cha Amali Makunduchi na kuona maendeleo ya ujenzi wa Chuo hicho ulioshindwa kukamilishwa kwa takriban miaka mine sasa.
Alisema tatizo kubwa linalolikabili ujenzi wa jengo hilo ni kutokuwepo kwa usimamizi imara, akibainisha miradi mingi ya Serikali kuzorota kwa sababu za kuleana.
Aliutaka uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanya tathmin ya matengenezo yaliofanyika, ili kujua thamani ya kazi iliofanyika, ikiwa ni hatua ya kumbana mkandarasi wa ujenzi huo, na kuona hatua gani za kuchukua, ikiwemo kuilipa Serikali.
Alisema kituo hicho ni muhimu katika maendeleo ya nchi, kwa vile kinatarajiwa kutoa wataalamu na kukidhi mahitaji ya kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitembelea barabara ya Kiwengwa – Mtende yenye urefu wa kilomita 4.7, ambapo Serikali imepanga kuijenga kwa kiwango cha Lami.
Alisema Serikali imetafakari na kuamua matengenzo yote ya barabara za ndani zifanyike kwa kiwango cha lami baada ya kubaini ujenzi wa barabara hizo kwa njia ya kifusi kuwa hauna tija.
Alisema barabara za ndani zenye urefu wa kilomoita 220 pamoja na barabara kuu zenye urefu wa kilomita 220 zote zitajengwa kwa kiwango cha lami, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikianao ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.
Vile vile Dk. Mwinyi alitembelea Hospitali ya Wilaya Makunduchi na kusema Serikali inalenga kuanzisha Hospitali zitakazoendana na hospitali husika pamoja na kuahidi kushughulikia maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo mishahara na maposho kwa kadri ya uwezo wa Serikali utakavyoimarika, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kunakuwepo utoaji bora wa huduma za afya nchini.
Aliwashukuru wafanyakazi wa Hospitali hiyo kwa juhudi kubwa wanazozichukua katika kutoa huduma, mbali na changamto mbali mbali zinazowakabili.
Nae, Mkurugenzi wa Mmalaka ya (ZAWA) Dk. Salha Mohamed Kassim alisema mipango ya ZAWA kwa mwaka wa fedha wa 2021 ni kupeleka miundombinu ya maji katika kituo kiliopo Kitogani kupitia mradi wa kisima cha Ras el hemma chenye uwezo wa kuzalisha lita za maji Milioni moja pamoja na kukiwekea Pump sahihi kituo hicho.
Alisema ongezeko la watu , sambamba na upungufu wa maji katika visima katika baadhi ya maeneo ndio sababu ya kuwepo changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Hadidi Rashid Hadidi, aliwasilisha taarifa za Utekelezaji wa shughuli za Maendeleo za Mkoa wa Kusini, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza changamoto kadhaa zinazoukabili Mkoa huo, ikiwemo migogoro ya ardhi.
Alisema changamoto kubwa za migogoro ya Ardhi zinazokabili Mkoa huo zinatokana na sababu tofauti, ikiwemo kutokuwepo kwa Hati ya matumizi ya Ardhi, eneo moja kumilikiwa na watu zaidi ya mmoja pamoja na ukosefu wa ufahamu wa matumizi sahihi ya eka tatu.