RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi jana usiku alikuwa mgeni rasmi katika taarab maalum iliyoandaliwa na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wawakilishi kwa kushirikiana na Benki ya NMB kwa ajili ya kumpongeza kufuatia ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020.
Taarab hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar ikiwa na madhumuni ya kumpongeza kwa ushindi mkubwa wa kishindo alioupata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huu 2020.Mapema kabla ya kuanza kwa taarab hiyo maalum, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid alitoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi Mkuu uliopita.
Aidha, alikipongeza Chama Cha Mpinduzi (CCM), kwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo huku akiipongeza Benki ya NMB kwa mashirikiano makubwa inayoyatoa hasa ikizingatiwa kuwa benki hiyo ni ya Serikali.
Nae naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdallah Juma Mabodi alitoa pongezi kwa Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa ushindi wake alioupata pamoja na chama chake cha CCM, na kueleza kwamba ushindi alioupata umetokana na dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.Aliongeza kuwa mashirikiano hayo yanayotolewa na Benki ya NMB ni muendelezo wa mambo aliyoyasisitiza Rais Dk. Hussein Mwinyi ya umuhimu wa kuwepo ushirikiano kati ya sekta binafsi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni.
Naibu Katibu Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kushirikiana na CCM katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.Mapema Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa ushindi wa kishindo alioupata huku akiahidi kwamba Benki ya NMB itaendelea kumuunga mkono yeye pamoja na kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi.
Alisema kuwa ushindi huo unatokana na imani kubwa waliyonayo wananchi kwa Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar.Pamoja na hayo, Zaipuna akieleza kwa niaba ya Benki yake ya NMB iliwapongeza Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid kwa kuchaguliwa kwa mara nyengine tena na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuliongoza Baraza hilo, aliwapongeza Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa ushindi walioupata.
Aidha, alieleza kuwa benki hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.Aliongeza kuwa benki hiyo ya biashara iko imara katika kutekeleza kazi zake ikiwa ni pamoja na kusaidiana na Serikali ya Awamu ya Nane kwani imejiandaa vyema na ina mtaji wa kutosha ambapo kwa upande wa Zanzibar tayari imeshafungua Matawi yake matatu yakiwemo mawili Unguja na moja liko kisiwani Pemba.
Alisema kuwa Benki hiyo ina ATM 17 na Mawakala zaidi ya 100 huku akieleza namna inavyoendeleza sekta ya utalii kwa kutumia kadi za Kimataifa “Union Pay International” (UPI) iliyoianzisha na Benki hiyo ambayo imekuwa ikisaidia sana hasa kwa watalii.Alieleza kwamba benki hiyo tayari imeshaanza kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane katika kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu kwa kuanza kufundisha wavuvi, wakulima wa mwani pamoja na watengeneza chumvi katika vijiji mbali mbali vya ukanda wa bahari.
Aliongeza kwamba katika zoezi hilo benki hiyo imeweza kufungua akaunti 50 kwa siku, imeweza kuwajengea uwezo akina mama na kuanza kuwakopesha fedha kuanzia laki 5 hadi milioni 5.Sambamba na hayo, Bi Zaipuna alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina asilimia 31.8 za hisa katika benki hiyo.Katika taarab hiyo maalum vikundi vya “Culture Music Club” na “Zanzibar Big Star” vilitumbuiza na kuonesha umahiri wao katika tasnia hiyo na kuifanya hadhira ishindwe kukaa vitini.
Nyimbo mbali mbali ziliimbwa na kikundi cha taarab asilia cha “Culture” ikiwemo Mpewa Hapokonyeki iliyoimbwa na Mgeni Khamis Abdalla, Wahoi iliyoimbwa na Sabina Hassan Khamis, Hongera Dk. Hussein Mwinyi iliyoimbwa na Mtumbwa Mbarouk na Kibali iliyoimbwa na Amina Abdalla.
Kwa upande wa kundi la “Zanzibar Big Star” lilionesha umahiri wake kwa kupiga taarab kwa mtindo wa kisasa na kuimba nyimbo mbali mbali ikiwemo Ngara CCM iliyoimbwa na Twahir Khamis, Zawadi iliyoimbwa na Fidia Said, Hongera CCM iliyoimbwa na Asha Khamis, Majaaliwa iliyoimbwa na Mwanaid Yussuf na nyenginezo.Katika taarab hiyo maalum, viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariyam Mwinyi pamoja na viongozi mbali mbali wa NMB kutokaka Makao Mkauu Dar-es-Salaam, viongozi wa CCM, Serikali, wanachama wa CCM na wananchi.