WANACHAMA na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) usiku wa jana walikonga nyoyo zao baada ya kikundi cha Culture Musical Club kutumbuiza katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, mjini hapa.Burudani hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar , ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ilikuwa na lengo la kumpongeza Dk. Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka CCM.
Katika taarabu hiyo nyimbo mbali mbali mpya na za zamani ziliimbwa na kuwafanya wapenzi wa muziki huo wa taarabu asilia kushindwa kujizuia vitini mwao muda wote.Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na ile ya ‘ pongezi kwa mgombea’ iliyoghaniwa kwa umahiri mkubwa na al-anisa Fatuma Dawa.
Nyengine ni ‘Mpewa hapokonyeki’ (al-anisa Mtumwa Mbarouk), ‘hongera Dk. Shein (ustadh Idd Suweid),’wahoi (al-anisa Sabina Hassan) pamoja na ‘Tunapendana iliyoghaniwa na mwimbaji maarufu al-anisa Fatma Abdisalami.Aidha, nyimbo nyengine ambazo ziliwafanya wasikilizaji kutabasamu na kuibuwa shangwe na nderemo ilikuwa ni pamoja na ‘Zanzibar ya Dk. Hussein Mwinyi’ iliyoimbwa na al-anisa Mgeni Khamis, ‘Haya maumbile yangu (al-anisa Amina Abdalla), ‘kama kupenda ni dhara (ustadh Idd Suweid) pamoja na ‘Mazoweya yana taabu iliyoghaniwa na al-anisa Fatma Dawa.
Katika hatua nyengine, mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka CCM, Dk. Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzungumza na washiriki wa burudani hiyo na kutoa shukuran za dhati kwa Dk. Shein kwa kuandaa burudani hiyo iliyofana sana.Alisema kwa kipindi chote tangu alipoteuliwa na Chama hicho kuwa mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar mjini Dodoma, ameendelea kupata mashirikiano makubwa na wanachama wa chama hicho, chini ya Uongozi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
Aidha, ameelezea kuridhishwa kwake na maandalizi ya kampeni yanayoendelea kufanyika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.Dk. Mwinyi aliahidi kuyaendeleza mambo yote mazuri yaliosisiwa na mtangulizi wake pamoja na kuweka ahadi ya kufanyika burudani ya aina yake baada ya chama hicho kufanikisha azma yake na kuingia Ikulu.
Ghafla hiyo iliyoandaliwa na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar pia iliwashirikisha viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mama Mwanamwema Shein, Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, mke wa Makamo wa Pili wa Rais, mama Asha Ali Idd pamoja na mke wa Mgombea Urais wa Zanzibar Mwinyi.