RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa eneo la Afrika Mashariki ni sehemu nzuri kiuchumi, iwapo utatumiwa vizuri ujuzi, maarifa, ubunifu pamoja na nyenzo zilizopo ili kukamilisha ndoto ya kufikia hadhi ya uchumi wa kati kitaifa na kikanda.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa maonyesho ya Wajasiriamali ya kuadhimisha miaka 20 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika huko katika viwanja vya Mji mpya wa Fumba, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja zina jumla ya watu zaidi ya milioni 162 jambo ambalo linatia moyo kwamba idadi hiyo ya watu inasadiia katika kujenga misingi madhubuti na mkubwa wa upatikanaji wa soko la bidhaa mbali mbali.

Alisema kuwa ukanda wa Afrika Mashariki una ardhi yenye ukubwa usiopungua kilomita za mraba milioni 1.82, na ikilinganishwa na pato la Taifa yaani GDP kwa nchi wanachama wanafikia jumla ya karibu Dola za Kimarekani Bilioni 79.

Hata hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa nyenzo mtambuka na muhimu ni ushirikiano wa pamoja katika jitihada za Wakuu wa Nchi za kuimarisha utawala bora jambo ambalo ni la msingi sana.

Alisema kuwa utangamano wa Afrika Mashariki umeweka vipaumbele vitano baina ya mwaka 2017 hadi 2021 ambapo miongoni mwa vipaumbele hivyo ni uimarishaji wa mzunguko huru wa utengenezaji na utoaji wa bidhaa miongoni mwa nchi hizo, uimarishaji wa maendeleo ya viwanda na kuongeza ubora katika bidhaa, usalama na utawala bora.

Aliongeza kuwa suala la kuendeleza viwanda limepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa ya kikanda na kimataifa.

Alieleza kuwa maonyesho hayafanywi kwa ajili ya kuangalia vitu, kuuza na kununua tu, bali ni kujifunza kwa njia mbali mbali, mbinu za kiufundi na mikakati ya kibiashara ili kuweza kuimarisha miradi mikubwa na midogo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefurahishwa sana na uamuzi uliochukuliwa wa kufanya maonesho hayo hapa Zanzibar katika Mji huo wa Fumba ambao ni aloama ya maendeleo makubwa ambao unaendelea kuimarishwa na mfanyabiashara mzalendo Sheikh Said Salim Bakhresa kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa hivyo, alisema kuwa maonyesho hayo yana umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya kuendeleza viwanda na kukuza shughuli ya ujasiriamali ambapo kwa mnasaba huo aliwahimiza washiriki wote wa maonyesho hayo kuitumia fursa hiyo ya maonyesho kwa kuelekezana, kushajiishana, kufundishana, kushirikiana na kujenga mtandao wa pamoja utakaowasaidia kati yao na wateja wao.

Alisema kwamba sekta ya viwanda ina umuhimu wa pekee katika ujenzi wa taifa ambapo maendeleo ya viwanda hulipelekea taifa kujitegemea katika kuyamudu mahitaji yake kiuchumi pamoja na kukuza ajira ambapo pia, viwanda vina umuhimu wa pekee katika kuwa na matumizi bora ya rasilimali zilizopo na zinazopatikana kutokana na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Hata hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuzingatia kwamba ili viwanda viendelee lazima pawe na masoko ya kutosha ya kuuza bidhaa na huduma zinazotolewa ambapo lengo moja la maonyesho hayo ni kuwakutanisha wateja, watengenezaji bidhaa pamoja na watoa huduma mbali mbali.

Alieleza kuridhishwa na mada waliyoichagua ya maonyesho hayo isemayo “ Sherehekea miaka 20 ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa kununua bidhaa zinazotengenezwa katika nchi zetu”.

Alisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kama ilivyo katika ujumbe wa mada hiyo, ndipo panapokuwa na masoko ya uhakika ya bidhaa zinazotengenezwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tuelewe kwamba tunapotengeneza bidhaa nchini huwa tunapunguza gharama za utengenezaji ambazo mara zote huingizwa kwenye bei anayolipa mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hizo….hata mimi nilipokuwa nikifunga maonesho ya Nne ya Wiki ya Wiwanda ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), niliweka mkazo juu ya kuvithamini vitu vyetu”, alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kufikiria mbinu bora zaidi zitakazoweza kutumika katika kuvisarifu vitu vya asili, viwe katika ubora na viwango vya juu ili viweze kuyavutia masoko tofauti ya ndani na nje.

Alieleza kuwa ubunifu ni jambo muhimu sana katika kuiendeleza miradi ya kibiashara na viwanda na kuondokana na ile fikra kwamba ujasiriamali ni kutengeneza bidhaa ndogo ndogo tu hizo kwa hizo na kuziuza.

“Kufanya hivyo, tunajikuta kwamba tumeivamia biashara moja au mradi mmoja tu sote, jambo ambalo linasababisha ufinyu wa soko”, aliongeza Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazochukuliwa katika kuwawekea fursa za mitaji na vifaa vijana ili waweze kujiajiri wenyewe.

Rais Dk. Shein pia, alieleza jinsi ya Serikali anayoiongoza katika suala zima la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ambapo alieleza jinsi ziara zake mbili za Kiserikali alizozifanya huko nchi za Falme za Kiarabu (UAE) Januari 2018 na Septemba 2019 jinsi zilivyoleta mafanikio.

Pia, alieleza jinsi Serikali ilivyotenga kiasi cha fedha cha TZS Bilioni 23 kama zilizotolewa na mfuko wa Khalifa Fund ili kutunisha zaidi msaada huo uweze kusaidia vikundi vingi vilivyokusudiwa hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa ujasiriamali ni sekta yenye manufaa makubwa kwa mtu, familia, jamii na taifa kwa jumla huku akieleza kuwa ujasirimali kama neno lenyewe lilivyo linahitaji ujasiri si jambo la kuvamia tu na badala yake mjasiriamali anatakiwa awe na mipango madhubuti ya nini anachokitaka kukifanya, wapi atapata mtaji na kiasi gani cha mtaji anachohitaji.

Alieleza imani yake ni kwamba mazuri watakayoyaona na kujifunza katika maonyesho hayo yatasaidia kujenga ari na hamasa ya kuingia katika sekta hiyo muhimu ya ujasiriamali ambapo pia, alitumia fursa hiyo kuwahimiza vijana bila ya woga wawe tayari kujiajiri katika kazi mbali mbali zenye heshima.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliihimiza Jumuiya ya (ZAFISO) kujenga itifaki na Jumuiya nyengine za Ujasiriamali ili waweze kujulikana zaidi na wao wawajue wengi zaidi na kuwataka wawe na wivu wa maendeleo.

Pamoja na hayo, alisisitiza amani na usalama katika nchi ndio msingi katika jitihada za kuendeleza viwanda, biashara na sekta zzote za kiuchumi na kijamii na kutaka kila mmoja achangie katika kuilinda na kuidumisha amani na usalama.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni jambo la faraja iwapo maonesho makuu ya maadhimisho ya kikanda ya kusherehekea kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2020 ambayo mara hii ni zamu ya Tanzania kama yatafanyika hapa Zanzibar.

Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico .alieleza mashirikiano makubwa yaliopo kati yao na Wizara yake na Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge pamoja na Jumuiya zote za Wajasiriamali na kuwapongeza kwa ushiriki wao mkubwa katika maonyesho hayo ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar.

Alitoa pongezi kwa wananchi wa Fumba pamoja na wananchi wengine wote ambao wanayaunga mkono maonyesho ya Wajasiriamali kwa kufika huko na kwenda kujionea na kununua bidhaa mbali mbali huku akitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Sheikh Said Salim Bakhresa kwa mashirikiano yake.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara yaKazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Fatma Bilali .alisema kwamba madhumuni makuu ya maonyesho hayo ni kuadhimisha miaka 20 ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na kuanzishwa kwa maonyesho ya Juakali ya Afrika Mashariki.

Malengo mengine alisema ni kusaidia kutangaza bidhaa za wajasiriamali ili waweze kupata masoko ya ndani na nje ya nchi, kukuza na kuimarisha biashara na ajira za wajasiriamali ili kuongeza kipato na kuwapunguzia umasikini pamoja na kuwajengea uwezzo wajasiriamali wa Zanzibar ili waweze kushiriki maonesho ya Jua kali ya Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa maonyesho hayo yamedhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na michango kutoka kwa baadhi ya Taasisi za Serikali na za Umma.

Alieleza kuwa maonyesho hayo yamezinduliwa leo na kuendelea hadi Novemba 24 mwaka huu ambayo yamewashirikisha wajasiriamali kutoka Tanzania Bara pamoja na Zanzibar ambapo jumla ya Wajasiriamali 183 na taasisi 17 zimeweza kushiriki katika maonesho hayo ambapo 75 ni kutoka Zanzibar na 108 kutoka Zanzibar.

Alielezaa kuwa maonesho hayo yameratibiwa kwa pamoja na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Biashara na Viwanda , Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ya SMT, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Jumuiya za Wajariliamali ya Tanzania Bara (CISO) pamoja na ya Zanzibar (ZAFISO).

Mapema akisoma risala ya Jumuiya ya Wajasiriamali wa Zanzibar (ZAFISO), Othman Bakari Sheha Mjasiriamali kutoka Pemba walieleza mashirkiano makubwa yaliopo katika Jumuiya yao na ile ya Tanzania Bara (SICO)  na kueleza kwamba dhamira za Jumuiya hizo ni kuwapatia taaluma na ujuzi wa uzalishaji mali, elimu, fursa za masoko kwa bidhaa zao na hatimae kujenga mtandao wa kiuchumi ili kukuza biashara zao na kukuza ajira kwa lengo la kuondokana na umasikini.

Alieleza kuwa jukumu jengine la Jumuiya hizo ni kuwaunganisha Wajasiriamali wote wanawake na wanaume na vijana ili kuwa na umoja, nguvu na sauti ya pamoja.

Hata hivyo, Wajasiriamali wa (ZAFISSO) walitoa ombi lao kwa wale wajasiriamali wanaoanza wapatiwe vitambulisho maalum ambavyo vitawaruhusu kufanya biashara zao kwa kulipa kiwango kidogo cha ada kwa kipindi maalum kama vile vinavyotolewa kwa Wamachinga huko Tanzania Bara. 

Wasanii mbali mbali walitumbuiza katika ufunguzi huo ambao ulihudhuria na viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya siasa wakiwemo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wananchi.