RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kila Idara ya serikali ina jukumu la kuhakikisha inafanya tafiti ili kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazojitokeza.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2019/2020.

Amesema sula la Utafiti haliihusu Idara ya Mipango, Sera na Utafiti pekee bali kila Idara ya serikali   ina jukumu la kufanya tafiti ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zilizopo.

Ameitaka Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuzishaijiisha Idara na vitengo mbali mbali vilivyomo katika Ofisi hiyo kufanya tafiti kwa mustakbali mwema wa maendeleo.

Amesema ili Idara au taasisi iweze kuendelea na kukabiliana ipasavyo na changamoto zinazoikabili, haina budi kujikita katika kufanya tafiti, ikiwa ndio njia muafaka katika kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto ziliopo.

Aidha, Dk. Shein amesema katika hatua za kuimarisha hali ya usalama Kisiwani Pemba, serikali inatarajia kuuwekea kamera za Usalama wa CCTV mji wa Chakechake.

Dk. Shein amesema utaratibu wa Bango Kitita umeisaidia sana Serikali kubaini changamoto mbali mbali na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati muafaka na kubainisha haja ya kuendelea kutumia utaratibu huo.

Amesema wakati uongozi wa awamu ya saba unaingia madarakani, kulikuwa na manung’uniko ya kuwepo bajeti ndogo katika Wizara zote za Serikali, jambo ambalo hivi sasa halipo, huku Wizara zote zikitekeleza vyema majukumu yake.

Aidha, Dk. Shein amesema Ofisi ya Rais ni kioo cha mafanikio, hivyo amewapongeza watendaji wa Ofisi kwa juhudi kubwa wanayoionyesha katika utekelezaji wa majukumu yao.

Nae, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwapongeza watendaji wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kufanyakazi kwa kujituma, kuwa waadilifu na waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aliwataka watendaji hao kuendeleza utamaduni huo, akibainisha hatua hiyo kuwa ndio chachu ya maendeleo.

Mapema, Waziri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ amesema katika kipindi hicho, Ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa programu zake, ikiwemo uandaaji wa jukwaa la sita la wana Diaspora wa Tanzania, huku serikali kwa upande wa Zanzibar ikiahidi kuliweka suala la wana diaspora kimkakati, kisera na kisheria.

Amesema katika kipindi hicho Ofisi ilifanikiwa kuendeleza ujenzi wa jengo la Ofisi yake liliopo Chakechake Pemba, ambalo kwa sasa limefikia hatua ya linta, wakati ambapo hatua za maandalizi ya kuliezeka zikiendelea.

Ameeleza kuwa Ofisi hiyo iliendelea kuratibu shughuli maalum ikiwemo kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi waliopata daraja la kwanza katika mitihani yao ya kidatu cha nne (2018) na sita 2019, hatua iliyomfanya Rais Dk. Shein kuongeza nafasi za udhamini wa masomo kwa wanafunzi bora kutoka wanafunzi 30 hadi 60.

Waziri Gavu amesema katika kipindi hicho Ofisi hiyo iliendelea kuchukua hatua ya kudhibiti mmong’onyoko wa udongo katika Ikulu ya Mkoani, wakati ambapo maeneo yalioathiriwa zaidi na mmong’onyoko huo yamedhibitiwa kwa kujengewa ukuta wenye urefu wa mita 35.

Aidha, amesema Ofisi ilifuatilia maagizo mbali mbali ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miradi ya barabara Unguja na Pemba, kama vile Kipapo – Mgelema yenye urefu wa kilomita 9.1 iliyowekewa kifusi katika maeneo yenye matatizo makubwa pamoja na barabara ya Ole – Kengeja.

Katika hatua nyengine, Waziri Gavu alimshukuru Dk. Shein kwa uongozi wake uliotukuka na wenye kushajiisha maendeleo nchini.

Nao, Washauri wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  wamempongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi kubwa anazochukuwa kuleta maendeleo nchini kupitia nyanja za kiuchumi na huduma za kijamii.

Wamesema katika uongozi wa Serikali ya awamu ya saba chini ya Uongozi wa Dk. Shein, Zanzibar imefanikiwa kupata maendeleo makubwa na kutajika ndnai na nje ya nchi.   

  • MKURUGENZI Mipango Sera na Utafiti Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Ndg Mwadini Haji akijibu swali wakati wa mkutano huo wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019 /2020, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. Ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein.(hayupo pichani)