RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeir, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, viongozi wa Serikali zote mbili, Viongozi wastaafu, Viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge,Wawakilishi, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, wananchi kutoka maeneo mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambayo ni miongoni mwa Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Zanzibar (Karume Day) ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na kuongozwa na Sheikh Jafar Abdallah kutoka Masjid Noor Muhammad.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Khamis Gharib kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana alitoa tafsiri ya Suratul Fussilat iliyosomwa na Ustadh Sharif Abdulrahman Muhidin kuanzia aya ya 30 mpaka aya ya 35 ambayo inaenda sambamba na maudhui ya siku hii ya leo.