RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana alikuwa mgeni rasmi katika taarab maalum iliyoandaliwa na vikundi mbali mbali vya Taarab vya hapa Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.
Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar ambapo viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali, wasanii pamoja na wananchi kadhaa walihudhuria akiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
Mapema wasanii hao wakisoma risala yao ya shukurani kwa Rais Dk. Shein, walimpongeza kwa kusimamia na kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka kumi huku akisimamia amani na utulivu sambamba na kuwajali wananchi wake wakiwemo wasanii.
Wasanii hao walieleza kuwa Rais Dk. Shein amefanya mambo mengi muhimu na mazuri katika kipindi chake cha uongozi akiwa Rais wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuunda Wizara maalum ya Vijana, Utawamaduni, Sanaa na Michezo ambayo iliwawezesha wasanii kukaa pamoja kwa kufanya kazi na kujadiliana mambo mbali mbali ya uchumi na maendeleo.
Jengine waliolieleza wasanii hao ni pamoja na kuwatengenezea studio ya kisasa ya kurikodi filamu na muziki, huko Rahaleo Jijini Zanzibar, studio ambayo imewawezesha kufanya kazi zao kwa ustadi mkubwa.
Wasanii hao walieleza kuwa Rais Dk. Shein ameweza kukiimarisha Kikundi cha Taifa cha Taarab kwa kukipa vifaa vipya na ofisi ya kufanyia kazi pamoja kurejesha maonyesho ya fensi ambayo yamewapa wigo mpana wasanii na kuwa wabunifu wa kazi mbali mbali za kisanii.
Aidha, wasanii hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuziunganisha Sheria za Baraza la Sanaa na Bodi ya Sensa na Filamu pamoja na kuwaangalia wasanii wagongwe na wagonjwa kwa kutembelewa na kuweza kusaidiwa.
Sambamba na hayo, wasanii hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwasaidia fedha maalum waasanii wote waliofika katika hafla hiyo huku wasanii wao wakionesha furaha yao kwa kumpa zawadi maalum Rais Dk. Shein kutokana na uongozi wake bora na uliotukuka.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Omar Hassan King akimkaribisha Rais Dk. Shein katika hafla hiyo alisema kuwa Taarab hiyo imeandaliwa na wasanii wa Taarabu kutoka vikundi tisa kikiwemo kikundi cha Taifa pamoja na vile vinavyojitegemea wakiwa na lengo la kumpongeza na kumuaga Rais wao.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa mara tu wasanii hao kumpelekea ombi Rais Dk. Shein la kutaka kumpongeza, Rais alikubali na kuruhusu vikundi vyote hivyo vitayarishe taarab hiyo ya kupongeza na kuahidi kushirikiana nao kama alivyofanya jambo ambalo limewapa faraja kubwa wasanii hao.
Mbali ya hayo, katika hafla hiyo wasanii hao pamoja na hadhara iliyokuwepo ukumbini hapo walitoa pongezi maalum ya siku ya kuzaliwa kwa Mama Mwanamwema Shein ambaye alionesha kushangazwa na kufurahia kitendo hicho ambacho hakutarajia.
Vikundi hivyo vya taarab viliweza kutoa burudani ya aina yake ikiwa ni miongoni mwa kutekeleza azma yao ya kumpongeza Rais Dk. Shein kwa mazuri mengi aliyowafanyia wao wasanii pamoja na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla.
Nyimbo zote zilizoimbwa katika hafla hiyo zilitia fora zikiwemo zile za kumpongeza Rais Dk. Shein na kuifanya hadhira kushindwa kutulia vitini hasa pale ilipoanza kuimbwa nyimbo ya kwanza yenye jina la “Cheo Chako”, iliyoimbwa na Al-Anisa Saada Mohammed wa kikundi cha Taifa kilichowajumuisha wasanii kutoka Unguja na Pemba.
Msanii Idd Suwedi ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya hafla hiyo alikuja na wimbo wake usemao “Kama Kupenda ni dhara” nyimbo iliyotiwa muziki na Abass Mzee na shairi lake kutungwa na Hija Saleh.
Kikundi cha Taarab cha Culture nacho kilitumbuiza nyimbo zake “Tumuenzi Dk. Shein” iliyoimbwa na Al-Anisa Fatma Dawa Shehe, “Umbo langu Dawa”, iliyoimbwa na Al-Anisa Mgeni Khamis Abdalla pamoja na wimbo wa “Mpewa Hapokonyeki” ulioimbwa na Al- Anisa Mtumwa Mbarouk.
Aidha, Kikundi cha Taarab asilia cha Naad Ikhwan Safaa nacho kilitumbuiza nyimbo zake ukiwemo “Khofu yako” uliyoimbwa na Profesa Mohammed Ilyas pamoja na wimbo “Hongera Dk. Shein ulioimbwa na Al-Anisa Fatma Hassan na Bi Baadie Omar Hamad.
Katika hafla hiyo pia, kikundi cha Rahat Zaman kinachopiga nyimbo za asili hasa zile zilizowahi kuimbwa na msanii Bibi Siti Binti Saad kiliimba nyimbo zake mbili ukiwemo wimbo wa “Ashki Baya” ulioimbwa na Kitukuu cha Bibi Siti Binti Saad Al-Anisa Muharam Mohammed.
Kikundi cha Mafunzo maarufu Wajelajela ambao hupiga taarab ya kisasa waliburudisha hadhara hiyo kwa wimbo wao “Hongera Dk. Shein”, nacho kikundi cha Wapendanao Modern Taarab kiliimba wimbo wake “Hongera Dk. Shein”, ulioimbwa na Al-Anisa Amina Kassim.
Sambamba na hayo, burudani hiyo iliendelea kwa kundi la taarab la Zanzibar One kuimba wimbo wake wa “Hongera Dk. Shein”, huku kundi la Diamond Modern Taarab kutoka JKU likitumbuiza wimbo wake wa “Shukurani Dk. Shein” ulioimbwa na Asha Imani Serumba na kundi la Big Star nalo likafanya vitu vyake kwa wimbo wa “Dokta wa Maendeleo”, uliomkusudia Dk. Shein ambao ulifunga dimba la hafla hiyo iliyonoga na kuwa kivutio katika usiku huo adhimu.