MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuridhishwa na kasi kubwa inayoendelea ya ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini “A”, Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Wazee wa CCM wa Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliwaleza wazee hao wa CCM pamoja na viongozi wengine wa chama hicho waliohudhuria katika mkutano huo kuwa kutokana na kasi hiyo kubwa ya ujenzi wa barabara hiyo yenye Kilomita za mraba 31 anamatarajio makubwa ya kuzinduliwa barabara hiyo katika sherehe za Mapinduzi zijazo.
Rais Dk. Shein alieleza na kushangazwa na juhudi kubwa zinazochukuliwa na mkandarasi wa barabara hiyo na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwasogezea huduma muhimu za kimaendeleo wananchi wake wote wa mjini na vijijini kwani hilo ndiolengo la Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja kwa wazee kuwaeleza vijana juu ya heshima ya wazee na vipi wazee wanatakiwa kuenziwa na kutunzwa sambamba na kupema heshima yao kutokana na mambo makubwa waliyoyafanya.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea kupatikana uhuru.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho, Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee ndio walioleta ukombozi na kuwakomboa wanyonge wa nchi hii hivyo ni vyema wakaendelea kuthaminiwa.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa na taarifa ya wazee hao wa Kaskazini A na kuahidi kuwa ahadi zote alizoziahidi katika Wilaya hiyo atazitekeleza na kuzifanyia kazi kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi.
Rais Dk. Shein alieleza haja kwa wazee kuwaeleza vijana na kuwafahamisha historia ya chama hicho pamoja na kuyarekebisha mambo ambayo yanaondoa mila, silka na desturi katika jamii.
Alieleza haja ya vijana kukumbushwa juu ya ukombozi wa Zanzibar ili wajue kwamba kazi hiyo imefanywa na wazee tokea kuanzishwa kwa ASP hadi Mapinduzi yaliyoongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Alieleza kwamba sio mambo yote yameandikwa katika vitabu lakini hakuna kitabu kizuri kama mzee na kusisitiza kwamba hakuna chama kilichoikomboa Zanzibar isipokuwa ni chama cha ASP.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya ukombozi wa Zanzibar na jinsi wazee walivyoshiriki kikamilifu katika kuhakikisha uhuru kamili unapatikana chini ya chama cha ASP.
Alisisitiza haja ya kuijua na kuifahamu historia ya Zanzibar hatua ambayo alisema ndio iliyomsukuma kuanza kuzungumza na wazee kwani wao wana historiakubwa hasa ikizingatiwa kwua wao ndio waanzilishi wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU.
Alieleza kuwa ushindi wa CCM katika chaguzi zake zote ni jambo ambalo halina mbadala hivyo, aliwaeleza wazee hao pamoja na wanachama wa CCM kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushika hatamu.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisisitiza kuwa CCM inathamani kuwepo kwa wazee na kueleza kuwa Serikali zote mbili zimeeleza jinsi zitakavyowajali wazee.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar kwa niaba ya wazee hao alimpongeza Rais Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kuwafuata wazee katika Wilaya zao Unguja na Pemba.
Naibu Mabodi alieleza jinsi ya uwepo wa Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote huku akieleza jinsi ya juhudi za Rais za ushirikishwaji wa Serikali na Chama pamoja na ushirikishwaji wa wananchi.
Nao Wazee wa Wilaya ya Kaskazini A, walimpongeza na kumshukuru Rais Dk. Shein kwa uongozi wake uliotukuka na jinsi anavyoendesha Serikali kwani wamepata matumaini na wameridhika sana na jitihada zake za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi wa mwaka 2015-2020 kwa vitendo.
Wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa ujenzi wa barabara mbali bali ndani ya Zanzibar hususan katika Wilaya ya Kaskazini “A” ambapo barabara zenyewe ni Mkokotoni hadi Kwanyanya, Matemwe, Kijini, Muyuni hadi Nungwi na Mkwajuni, Kiongele hadi Pale.
Kwa upande wa sekta ya afya wazee hao walipongeza kwa kuipandisha hadhi Hospitali ya Kivunge kuwa Hospitali ya Wilaya pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mbuyumaji.
Wakieleza kuhusu sekta ya elimu wazee hao walitoa pongezi kwa Makamo Mwenyekiti hyo wa CCM Zanzibar kwa kujengewa Skuli ya Mlilile pamoja na Skuli ya Mbuyumaji zote zilizomo katika Wilaya yao.
Wazee hao waliahidi kuendelea kukitumikia chama hicho kwa gharama yoyote ile pamoja na kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Pamoja na hayo wazee hao wa Wilaya ya Kaskazini “A” walimpongeza Rais Jon Pombe Magufuli kwa kuendeleza kasi kubwa ya maendleo ya kuijenga Tanzania na kumuomba azidi kuudumisha Muungano ambao sasa umetimiza miaka 55 tangu kuasisiwa kwake.
Waliongeza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana katika Wilaya yao kutokana na Utekelezaji huo wa Ilani ya Uchagizi ya CCM ni pamoja na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji safi na salama Chaani Masingini, maji safi na salama katika vijiji vya Mbuyumaji na Mlilile.
Aidha, mafanikio mengine ni mradi Mkubwa wa umeme wa Kijini, Mbuyutende, Mbuyumaji na Mlilile pamoja na kuwapatia Pencheni jamii Wazee wapatao 4,161 wenye umri wa miaka 70 katika Wilaya yab Kaskazini A.
Wazee hao pia, walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendeleza kwuapatia Pencheni Wastaafu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wastaafu wa kiwanda cha Sukari Mahonda.
Kwa upande wa TASAF Wazee hao walieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawapatia Kaya Masikini 4227 jumla ya TZS milioni 147.548,000 kila baada ya miezi miwili wananufaika na fedha hizo.
Nae Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “A”, Ali Khamis alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kusimamia vyema madhumuni na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuendelea kukiimarisha chama hicho cha (CCM).
Pia, Mwenyekiti huyo alieleza jinsi wananchi wa Wilaya ya Kaskazini A, walivyofarajika kwa ujenzi alioufanya wa Tawi lililoanza kujengwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume huko Mshezashauri pamoja na ujenzi wa Maskani mbali mbali za CCM katika Wilaya hiyo.
Aidha, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo alitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kusimamia na kuuendeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar sambamba na kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa hapa nchini ambao umepelekea kuwepo kwa maendeleo endelevu.