RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa mkono wa pole kwa familia ya Marehemu Mzee Haji Nasibu Haji Nyanya aliyefariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumamosi ya Julai 11, 2020 huko Jijini Dodoma.

Rais Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu haji Nasibu Nyanya mara tu baada ya kurejea Jijini Dodoma ambako alishiriki katika vikao mbali mbali vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akiwa nyumbani kwa Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya huko Bububu, Rais Dk. Shein aliwapa mkono wa pole wanafamilia wote akiwemo mjane wa Marehemu Bi Zainab Nyanya na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Rais Dk. Shein akiwa amefuatana na Mama Mwanamwema Shein aliitaka familia hiyo kumuombea dua Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya ambaye alikuwa ni mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara wa muda mrefu.

Nayo familia ya Mzee Nyanya ilitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kushirikiana nao bega kwa bega katika msiba huo yeye pamoja na Mama Shein ikiwa ni pamoja na kwenda kuwapa mkono wa pole mara tu baada ya kurudi safari.