Salamu hizo za pongezi zilieleza kuwa kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar anatuma salamu za pongezi kwa Rais Obama kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo.Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Marekani wameona umuhimu wa kumuunga mkono Rais Obama na kumrejesha tena madarakani kwa lengo la kuliendeleza na kuliongoza taifa hilo kubwa duniani kwa kipindi cha miaka mine ijayo.
Pamoja na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na rafiki zao wa Marekani katika kusherehekea ushindi huo uliotokana na uchaguzi mkuu wa hivi karibuni wa Marekani ambao umempa ushindi Rais Obama.Dk. Shein alimtakia uongozi mwema Rais Obama na kutoa salamu za pongezi kwa familia ya Rais Obama akiwemo Mkewe Mama Michelle Obama na watoto wake wote Malia na Sasha Obama pamoja na wananchi wa Marekani ambao wameonesha wazi imani na uaminifu mkubwa walionao katika uongozi wa Rais Obama.Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Marekani utazidi kuimarika.