Media » News and Events

Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), yatawezesha kutambua na kutathmini mchango, maendeleo ya Umoja huo pamoja na nafasi ya wanawake.

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akimsikiliza Mjasiriamali wa Kikundi cha Chuo cha Wajasiriamali Wilaya ya Mjini kinachojishughulisha na utengenezaji wa losheni Bi.Rauhiya Abdalla Khamis, wakati akitembelea maonesho ya Wajasiriamali Wanawake wa Wilaya ya Mjini Unguja katika Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) yaliofanyika katika viwanja vya Kituo cha Amali Miembeni na (kulia kwake) Makamu Mwenyekiti wa UWT Mhe Thuwaiba Editon Kisasi.

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), yatawezesha kutambua na kutathmini mchango, maendeleo ya Umoja huo pamoja na nafasi ya wanawake katika ujenzi na uimarishaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali na jamii kwa jumla.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa ya maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) 2021, kwa Wilaya ya Mjini, hafla iliyofanyika katika ukumhi wa skuli ya Chekechea Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Katika maelezo yake, Mama Mariam Mwinyi alisema kuwa mkusanyiko wa pamoja kati ya viongozi wa Jumuiya ya (UWT), Jumuiya nyengine za (CCM), Viongozi wa Serikali na wanachama wa (CCM) una maana ya kusherehekea na kutathmini maendeleo yanayoendelea kupatikana katika nyanja ambali mbali hapa nchini.

Alieleza jinsi alivyovutiwa na madarasa ya Ujasiriamali yaliyopo katika eneo hilo la skuli ya Chekechea Miembeni ambayo yameanzishwa kwa ajili ya kutoa elimu ya Ujasiriamali kwa vijana wa kike na kiume ambao hawakubahatika kuendelea na elimu ya Sekondari pamoja na wale wasioweza kujikimu kimaisha wakiwemo wanawake wajane wenye kipato kidogo.

Alisema kuwa juhudi za (UWT) katika kuimarisha elimu ya Ujasiriamali zinaenda sambamba na dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuzaa nafasi za ajira 300,000 ifikapo mwaka 2025.

Mama Mariam Mwinyi alisisitiza kwamba juhudi zinazochukuliwa na (UWT) katika kuimarisha chuo hicho na shughuli za Ujasiriamali lazima zizingatie mambo matatu muhimu ambayo yamekuwa yakisisitizwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ambayo ni elimu, mitaji na masoko.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane hivi sasa inakamilisha taratibu za kuunganisha mifuko yote ya ujasiriamali kuwa Mfuko mmoja imara ikiwa na lengo la kuhakikisha kwamba panakuwa na mfuko mmoja wenye nguvu na uwezo mkubwa wa kutoa mikopo nafuu kwa wakundi mbali mbali ya Wajasiriamali.

“Vile vile,  inajenga matumaini kuona kwamba, Benki na taasisi za fedha zinaendelea kujitokeza kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuimarisha ujarisiamali kwa kuwa tayari kutoa mikopo yenye gharama nafuu. Ni wajibu wetu sasa kuhakikisha kwamba, tunazitumia fursa hizo kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu ili vikundi tunavyoviunda viwe vinaaminiwa na vinakopesheka”,alisema Mama Mariam Mwinyi.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi aliwataka viongozi na wanaCCM kuupokea vizuri uchumi wa Buluu kwa kuanzisha vikundi vitakavyoshughulikia na kuimarisha kilimo cha mwani,  kuendeleza uvuvi wa kisasa pamoja na utalii sanjari na kujitayarisha kuipokea vizuri sekta ya mafuta na gesi na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha bandari huku akiupongeza uongozi wa chuo kwa kuanzisha darasa la kujifunza kuhusiana na uchumi wa buluu.

Alisisitiza haja kwa uongozi wa Chuo hicho kutilia mkazo utoaji wa elimu ya itikadi na uzalendo huku akieleza jukumu la Chama na Jumuiya zake katika kuhakikisha kwamba wanawaandaa vyema vijana kwani wao ndio warithi wa Taifa la kesho.

“Kwa pamoja tuhakikishe tunawapa malezi bora watoto wetu na tunashirikiana katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia na utumiaji wa dawa za kulevya”,alisema Mama Mariam Mwinyi.

Pamoja na hayo, kwa upande wa watoto wa kike, Mama Mariam Mwinyi alieleza haja ya kuwakinga na tatizo la mimba za utotoni ambazo huathiri elimu na mwelekeo mzima wa maisha yao.

Mama Mariam Mwinyi, aliwasisitiza wazazi na walezi kuwatunza na kuwalinda watoto juu ya susla zima la unyanyasaji wa kijinisia na kuwa wajasiri katika kutoa taarifa kwa Serikali iliyopo madarakani ambayo ni sikifu ambapo hivi sasa hatua za makusudi imekuwa ikichukua kukomesha janga hilo.

Pia, aliitaka Jumuiya ya (UWT) kujipanga na kutekeleza mikakati mipya itayowezesha kufanya kazi kwa karibu zaidi na wanawake wajane na Jumuiya zao kwani hivi sasa ongezeko la wanawake walioachwa na kutelekezwa na watoto kila uchao linazidi.

Nao viongozi wa UWT, Wilaya, Mkoa na Taifa walimpongeza Mama Maria Mwinyi kwa kukubali kuungana nao katika maadhimisho hayo huku wakieleza shughuli mbali mbali ambazo wamezifanya kuanzia kisiwani Pemba tokea Septemba 28, 2021 na wanaendelea nazo hadi Oktoba 04, mwaka huu zikiwemo kusaidia Jamii.

Nae Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Ujasiriamali kiliopo hapo Miembeni Mjini Unguja Said Kheri Ame, alisema kuwa chuo hicho kilichoanzishwa Mei 06, 2019 kimekuwa kikitoa mafunzi mbali mbali kwa wanawake, wanaume wakiwemo vijana wa kike na kiume ambao hawakubahatika kuendelea na elimu ya Sekondari pamoja na wale wasioweza kujikimu kimaisha wakiwemo wanawake wajane wenye kipato kidogo.

Mapema, Mama Mariam Mwinyi alitembelea madarasa ya wanafunzi Wajasiriamali wanaosoma katika Chuo hicho kinachosimamiwa na UWT hapo Miembeni na kupata maelezo juu ya shughuli na bidhaa mbali mbali wanazotengeneza na mwisho wa hotuba yake aliwakabidhi vyeti wahitimu wa mafunzo hayo.