MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameiunga mkono kauli ya Wazee wa CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja ya kuwa Mkoa huo utaendelea kubaki kuwa ngome ya CCM.
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati alipofanya mazungumzo na Wazee wa Wilaya ya Kusini Unguja na Wazee wa Wilaya ya Kati Unguja wakati akihitimisha ziara zake za kukutana na Wazee wa CCM wa Wilaya zote za Zanzibar.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa Wilaya ya Kusini Unguja ina historia kubwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo, anaamini kuwa Wilaya hiyo ina uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa ngome ya chama hicho.
Alieleza kuwa ushindi wa CCM katika chaguzi zake zote ni jambo ambalo halina mbadala kwani hilo ni agizo la Katiba ya Chama hicho kutokana na malengo iliyojiwekea.
Alisema kuwa malengo ya CCM yako wazi kwamba chama hicho kimeundwa kwa lengo la kushinda uchaguzi Mkuu na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, aliwataka viongozi wa CCM wale wote walioko madarakani na wale wasiokuwepo madarakani kujua kwamba bado wana nafasi ya kukipigania Chama hicho kama wanavyofanya Wazee na Mabaraza yao pamoja na Jumuiya za Chama hicho.
Aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kufanya kazi na wazee sambamba na kuwasaidia ili waendelee kukiimarisha chama.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja kwa wazee kuwaeleza vijana juu ya heshima ya wazee na vipi wazee wanatakiwa kuenziwa na kutunzwa sambamba na kupewa heshima yao kutokana na mambo makubwa waliyoyafanya.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea kupatikana uhuru wa Tanganyika na uhuru wa Zanzibar kupitia vyama vya ASP na TANU.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee ndio walioijenga Zanzibar na kuleta ukombozi na hatimae kuwakomboa wanyonge wa nchi hii.
Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ipo haja ya kupokea mawazo ya wazee sambamba na kuwaheshimu na kuwalinda wazee kwani kuna kila sababu ya kufanya hivyo hasa ikizingatiwa historia ya wazee katika kupigania uhuru wa nchi hii.
Rais Dk. Shein alipongeza kwa mapokezi makubwa aliyoyapata katika Wilaya hiyo na kuipongeza risala iliyotolewa ambayo imetoa pongezi kwake na kwa Serikali pamoja na wananchi kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.
Makamu mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza umuhimu wa wazee umo kwenye Katiba na Ilani ya CCM kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliongeza kuwa wakati huu uliopo ndio wakati mzuri wa kushikamana na kuwa kitu kimoja sambamba na kuongeza nguvu katika kukiimarisha na kukiendeleza Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisisitiza kuwa ushindi kwa CCM ni lazima ili Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 yaendelee kulindwa yadumishwe na yaendelezwe sambamba na kudumishwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alieleza kuwa utamaduni wa Rais Dk. Shein wa kukutana na wazee ameuanza muda mrefu na kusisitiza haja kwa viongozi wengine wa chama kuiga utamaduni na utaratibu huo.
Naibu Mabodi alieleza kuwa mbali ya juhudi alizozichukua katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo nchini pia, amefanya juhudi katika kukiimarisha chama kwa kujenga Matawi, kuimarisha Mashina pamoja na Ofisi za chama.
Nao Wazee wa Mkoa wa Kusini Unguja walimuaahidi Rais Dk. Shein kuwa Mkoa huo utaendelea kubaki kuwa ngome ya CCM.
Kwa upande wao Wazee wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja walieleza kuwa wanaamini kuwa ujio wa Rais Dk. Shein katika Wilaya hiyo watapata baraka, nasaha, busara pamoja na hekima zake za kuijenga CCM hususan kwa kipindi hichi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Aidha, walieleza jinsi wanavyoridhika na utekekelezaji wa Rais Dk. Shein wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa vitendo pamoja na ahadi zake alizozitamka kipinndi cha Kampeni zilizopita kuzitimiza.
Wazee hao walimpongeza kwa mengi aliyoyafanya ndani ya Zanzibar kwani yapo ambayo yamewagusa moja kwa moja ikiwa ni pamoja na malipo ya Pencheji Jamii ya TZS 20,000 ambapo walianza wazee 1,421 mnamo mwaka 2016 na hivi sasa wapo wazee 1,348 ambao wote wanapata Pencheni hiyo.
Pia, wazee hao walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kwa jitihada na huruma zake kubwa aliyowaonesha wazee kwa kuwaongeza kima cha chini cha penscheni ya wastaafu.
Walieleza kuwa uungwana wa uchapakazi wa Rais Dk. Shein uliotukuka wao wazee wanauona zaidi pale alipolisimamia kidete suala la upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya yao na kutolea mfano wa kutatua tatizo la maji Makunduchi eneo la Mnywambiji.
Aidha, ahadi aliyoitoa Shehia ya Mtende ameitimiza kabla ya muda wake aliouahidi kufika sambamba na kero ya muda mrefu Shehia ya Michamvi nayo ameshaipatia muarobaini wake na sasa kazi ya kuzika mabomba inaendelea kutokea katika visima vya Ras el Khaimah Bwejuu kuelekea Michamvi.
Walieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kugharamia zaidi ya Bilioni 1.8 katika mradi huo.
Pia, wazee hao walieleza kuridhika na juhudi anazozichukua na Serikali anayoiongoza katika suala zima la kipaumbele cha elimu kwa Zanzibar nzima, kuanzia ujenzi wa skuli za ghorofa, mipango imara ya kuendesha elimu, ufaulu wa wanafunzi umeongezeka na utoro wa skuli umepungua.
Sambamba na hayo, wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwajengea Chuo Cha Amali killichopo Kisongoni Makunduchi na Skuli Sekondari ya kisasa iliyopo Kibuteni, kuwepo kwa majengo hayo wanaamini itatoa viongozi bora wa hapo baadae.
Kwa upande wa sekta ya afya wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuifanya Wilaya yao ya Kusini kuwa na huduma za kisasa na zinazokwenda na wakati kwa kuipandisha hadhi Hospitali yao ya Makunduchi kuwa Hospitali ya Wilaya.
Walieleza kwamba kufanya hivyo kunasaidia kwa kiasi kikubwa baadhi ya huduma ambazo walilazimika kwenda katika hospitali ya rufaa na sasa zimesogea Hospitalini hapo.
“Tunashukuru sana wazee wako kwa hakika wewe ni mja mwema unaejali wazee wako bila ya ubaguzi wa rangi, kabila wala itikadi ya siasa tunasema ahsante sana”, walieleza wazee hao kwenye taarifa yao hiyo.
Nao Wazee wa Wilaya ya Kati Unguja kupitia Baraza lao la Wilaya ya Kati kwa namna ya kipekee waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba anaoiongoza Rais Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kizalendo wa kuwapelekea huduma mbali mbali za kijamii.
Wazee hao walieleza kuwa suala zima la Pencheni Jamii ya kila mwezi wanayoipata wazee wapatao 1977 wa Wilaya ya Kati jambo ambalo kwao ni faraja ambayo hawakuitegemea.
Walieleza kwamba fedha hizo zinawasaidia kufanya shughuli ambazo zinawainua kiuchumi na kuachana na utegemezi kwani hayo ndio madhumuni ya ASP chini ya uongozi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Kwa upande wa sekta ya afya, wazee hao walieleza kuwa wanafaidika na ujenzi wa vituo vipya vya mama na mtoto katika Shehia ya Umbuji, Mwera, Kiboje, Mkwajuni, Bambi na Tunguu.
Aidha, kwa upande wa sekta ya elimu wazee hao walieleza kuwa wamefaidia kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hiyo kutokana na kujengewa skuli za Sekondari za kisasa katika Shehia ya Uroa skuli ya ghorofa, skuli ya Uzini, Tunguu pamoja na maabara kubwa katika skuli ya Unguja Ukuu kaepwani.
Wazee hao wa Wilaya ya Kati walitoa shukurani zao kwa wakulima kuendelea kusaidiwa ambapo Serikali imebeba asilimia 70 ya gharama za pembejeo na wakulima kulipia asilimia 30.
Pamoja na hayo, wazee hao walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuitekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzii ya CCM wka kuyabadilisha Mabonde yao ya mpunga kwenda na teknolojia ya Kisasa kuyafanya ya umwagiliaji maji na kupata eka 2095 katika mabonde ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wa mifugo wazee hao walieleza jinsi walivyofaidika na mradi wa “Kopa ngombe lipa ngombe” kwa kwuaongezea kipato wafugaji na kuifanya Wilaya hiyo kuwa ni moja ya watoaji wa maziwa kwa wingi ambapo kwa mwezi wanakusanya lita 31068.
Wazee hao walitoa pongeza kwa Rais Dk.Shein kwa kuwarahisishia harakati zao za maisha kuwa nyepesi kwa kuwajengea barabara kila upande katika Wilaya yao ikiwemo barabara ya Jendele hadi Unguja Ukuu, Koani hadi Jumbi, Umbuji hadi Uroa, Ukongoroni, Charawe hadi Bwejuu ambayo inaendelea kujengwa.
Kwa upande wa huduma ya maji, wazee hao walieleza kufurahishwa na ukarabati wa Matangi ya maji Unguja Ukuu kwani hatua hiyo itawafanya watu wa kisiwa cha Uzi na Ng’ambwa kuwa na matumaini ya kupata maji safi na salama.
Wazee hao pia, walishukuru sana kwa kuanzishwa utaratibu mpya wa kuwakumbuka na kuwaombea dua Waasisi na viongozi mbali mbali ambao wamelitumikia Taifa hili kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Nao wenyeviti wa CCM Wilaya ya Kusini na Wilaya ya Kati Unguja walipongeza ukusanyaji wa mapato na ukuaji wa uchumi jinsi ulivyoimarika hapa Zanzibar hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa huduma mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na ununuaji meli mpya ya mafuta na meli ya abiria.
walimpongeza Makamo huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Rais Dk. Shein pamoja na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Magufuli kwa hatua walizochukuwa katika kuhakikisha ada kwa wanachama wa CCM inahifadhiwa katika akauti maalum hatua ambayo imepelekea kupatikana fedha nyingi.