RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba na kisheria katika kulinda amani, utulivu na maisha ya wananchi na mali zao.

Dk. Shein amesema hayo Uwanja wa Amani mjini hapa, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa mikao mitano ya Zanzibar, katika kilele cha maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema suala la kudumisha amani halina mbadala, hivyo akasisitiza kuwa Serikali haitochelea kumchukulia hatua mtu yeyote atakaejaribu kuhatarisha amani ya nchi.

Aidha, Dk. Shein alisema mpango kazi wa miaka mitano wa kumaliza vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto uliozinduliwa Agosti 2017 umeanza kuonyesha mafanikio, sambamba na mwamko kwa wananchi kuongezeka kwa kuripoti matukio hayo.

Alisema jumla ya matukio 1,091 ya udhalilishaji yaliripotiwa katika vituo vya Polisi Unguja na Pemba mwaka 2017/2018, ikilinganishwa na matukio 2,449 mwaka 2016/2017, ikiwa ni upungufu wa matukio 1358, sawa na asilimia 124.5.

Dk. Shein alisema vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua na kufikia 155 kwa kila vizazi hai 100,000, ikilinganishwa na vifo 288 kwa kila vizazi hai 100,000 katika mwaka 2010.

Alisema jitihada za kuwaelimisha mama wajawazito kujifungulia hospitali badala ya majumbani zimesaidia sana ambapo mwaka 2010 wajawazito 51,912 walijifungulia majumbani ikilinganishwa na 37,803 mwaka 2019.

Vile vile, Dk. Shein alisema maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi yameeendelea kushuka na hivi sasa yamefikia kiwango cha asilimia 0.4 kutoka asilimia 0.6 mwaka 2010.