RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu na kumchagua mgombea wa Urais wa Chama hicho Dk. Hussein Mwinyi, ili kutimiza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.
Dk. Shein ambae pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, amesema hayo katika viwanja vya Kibandamaiti Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati akifunga Kampeni za Chama hicho zilizodumu kwa takriban siku 45.
Amesema kitendo cha wananchi hao kujitokeza kwa wingi na kuwachagua wagombea wote wa CCM ni hatua ya kuyatetea Mapinduzi ya 1964 yalioleta heshima, uhuru na ukombozi kwa Wazanzibari.
Mapema, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, akiwa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi amesema endapo Wazanzibari waamchagua, watakuwa wameandika Historia ya kumchagua Rais wa kwanza aliezaliwa baada ya Mapinduzi 1964, na hivyo kukidhi mahitaji ya wakati katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zilizopo hapa nchini.
Dk. Mwinyi ameahidi kuimarisha uchumi wa Zanzibar, kupitia uchumi wa Buluu ambamo ndani yake amesema kuna sekta mbali mbali kama vile, Utalii, mafuta na gesi asilia na kadhalika, sambamba na kufanikisha ujenzi wa Bandari kubwa ili kuibua ajira kwa vijana.
Aidha, mgombea huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, viongozi mbali mbali Chama hicho pamoja na wananchi wote kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za chama hicho hadi kufikia kikomo chake.
Nae, Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema njia pekee ya kulinda tunu na urithi ilioachwa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 ni kuwapigia kura wagombea wa CCM, hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi, sambamba na kuweka pembeni tofauti zilizojitokeza wakati wa mchakato wa kupata wagombea.
Aidha, Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amempongeza Rais Dk. Shein kwa kazi kubwa na nzuri na inayopimika aliyoifanya katika kipindi chote cha uongozi wake na kuondoka akiiwacha Zanzibar ikiwa na amani na utulivu.
Kampeni za Chama cha Mapinduzi zilizinduliwa rasmi Agosti 29, mwaka huu katika Uwanja wa Jamuhuri mjini Dodoma na Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Joseiph Pombe Magufuli.