RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi ameipongeza azma ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulkia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa jengo la Beit al Ajaib baada ya kuporomoka sehemu kubwa ya jengo hilo hivi karibuni.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tirso Dos Santos.Rais Dk. Mwinyi alimueleza Mwakilishi huyo wa (UNESCO) kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Shirika hilo, hivyo hatua yake hiyo ya kuinga mkono Zanzibar katika kulifanyia matengenezo jengo la Beit al Ajaib ni uthibitisho mkubwa.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kuchukua hatua za makusudi mara tu baada ya kutokea tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati ya Uchunguzi ya sababu zilizopelekea kuanguka kwa jengo hilo la Beit al Ajaib huku yeye mwenyewe akikutana na Wadau wa Mji Mkongwe kujadili tukio hilo kwa azma ya kutafuta ufumbuzi.

Rais Dk. Mwinyi alitoa ushauri kwa Shirika la (UNESCO) wa kuyafanyia tathmini majengo yote ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ili yasiendelee kuleta athari zaidi.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa azma na utayari wa Shirika la (UNESCO) wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kulijenga jengo hilo la kihistoria ina umuhimu mkubwa katika kuurejeshea hadhi yake Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika urithi wa dunia.

Pia, Rais Dk. Mwinyialifurahishwa na azma ya Shirika hilo la kuwaleta wataalamu kwa awamu tatu hapa Zanzibar ambapo kila awamu itakuwa na wataalamu wake ambapo inaonesha azma sahihi ya (UNESCO) ya kushirikiana na Zanzibar katika kulijenga tena jengo hilo kwa mtazamo wake wa asili na kwa kiwango kilicho bora zaidi.Aidha, Dk. Mwinyi alimueleza Mwakilishi huyo wa (UNESCO) kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa timu hizo za wataalamu watakaokuja kufanya shughuli hiyo hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya shughuli zao.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi kwa upande mwengine alilipongeza Shirika hilo kwa azma yake ya kulifanyia ukarabati jengo la sinema ya Majestic ambapo tayari nusu ya fedha za ujenzi huo kwa mujibu wa Mwakilishi huyo zimeshapatikana.Alieleza kuwa Shirika hilo limeweza kushirikiana na Zanzibar kwa muda mrefu hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa miradi mbali mbali ambayo (UNESCO) inaiunga mkono ikiwemo miradi ya elimu, utamaduni, afya na mengineyo ambayo imepata mafanikio makubwa hapa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika hilo ili kutekeleza malengo yaliokusudiwa.Mapema na Mwakilishi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tirso Dos Santos, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kuwa Shirika hilo lina azma ya kulifanyia ma   ujenzi jengo la Beit-al -Ajaib ili lirudi katika uhalisia wake kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwakilishi huyo, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kuwa Shirika hilo litaanza kuleta wataalamu wake kwa ajili ya mradi huo ambao wataanza kuja mnamo Januari 18 mwaka huu ambao watakuja kwa awamu tatu ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafanikiwa tena kwa muda uliopangwa na ufanisi mkubwa.Alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba (UNESCO) itahakikisha inafuata taratibu zote katika kuhakikisha ujenzi huo ufanywa kwa taratibu zote za Kimataifa bila ya kuathiri mambo mengine.Pia, Mwakilishi huyo wa (UNESCO), alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba baada ya timu hizo za wataalamu kukamilisha kazi zao ujenzi wa jengo hilo utaanza mara moja huku akimueleza kuwa amepokea ushauri na wazo la kuyafanyia tathmini majengo ya Mji Mgongwe wa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Mwakilishi huyo wa (UNESCO), alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Shirika hilo liko tayari kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la sinema ya Majestic ambalo limo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar na tayari nusu ya fedha za ukarabati wa jengo hilo ziko tayari.

Mwakilishi huyo alimpa salamu za rambi rambi zilizotumwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bi Audrey Azoulay pamoja na Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Urithi wa Dunia Bi Mechtild Rossier kufuatia kuporomoka kwa jengo la Beit al Ajaib na kupelekea vifo pamoja na mejeruhi kadhaa.Sambamba na hayo, kiongozi huyo alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 huku akisisitiza (UNESCO), itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbali mbali ili iweze kuleta tija na ufanisi.

Sehemu kubwa ya jengo la Beit el Jaaib liliopo Forodhani Jijini Zanzibar ambalo ni miongoni mwa majengo ya urithi wa dunia ambapo pia, ni miongoni mwa majengo yanayotambuliwa na (UNESCO) liliporomoka Ijumaa ya Disemba 25, mwaka jana 2020 likiwa linaendelea kufanyiwa ukarabati.