SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuregeza masharti iliyoyaweka hapo awali katika mambo kumi ya kuyadhibiti maradhi yanayosababishwa na maambukizi ya virusi vya Corona hatua kwa hatua.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo leo katika hotuba yake ya Baraza la Idd El Fitri aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari baada ya kukamilisha ibada ya saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa salama na amani.

Katika maelezo yake Alhaj Dk. Shein alisema kuwa uwamuzi wa kuregeza masharti hayo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utatolewa wakati wowote kuanzia hivi sasa.Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa tamko rasmi tarehe 19 Machi, 2020 juu ya ugonjwa wa COVID-19 hapa Zanzibar na kutoa mambo kumi ya kutekelezwa katika kuwahudumia waathirika wa maradhi hayo sambamba na kuyadhibiti maambukizo yake.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali imefarajika kuona namna wananchi walivyokuwa imara katika kupambana na COVID-19 kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha maambukizo katika sehemu zote Unguja na Pemba.Alieleza kuwa hadi tarehe 20 Mei, 2020 jumla ya wagonjwa 34 walioambukizwa maradhi hayo wanaendelea kupata matibabu katika vituo vitano vilivyoanzishwa kutoka miongoni mwa idadi ya wagonjwa 134 iliyowahi kufikiwa tarehe 1 Mei, 2020 na kueleza kuwa wagonjwa wote wanaendelea vizuri na hakuna mwenye hali mbaya.

“..........inatupasa tuongeze nguvu katika kutumia umoja wetu na mshikamano tulionao, maelewano, bidii, subira na tuendelee kushirikiana katika kupambana na ugonjwa huu na katika ibada zetu tuendelee kumuomba Mola wetu Mtukufu kama tunavyomuomba wakati wote ili atupe ushindi katika vita hivi na atukinge na kila janga na balaa”, alisisitiza Alhaj Dk. Shein.Aidha, Rais Dk. Shein kwa mara nyengine tena alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kupambana na Maafa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ambaye pia ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Pia, alimpongeza Mwenyekitiwa Kamati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupambana na Maradhi haya ya COVID-19, Kassim Majaaliwa Majaaliwa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wajumbe wao wote kwa kufanya kazi kwa kushrikiana na uzalendo wa hali ya juu.Alhaj Dk. Shein alitoa pongezi kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid pamoja na Wawakilishi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.

Aliwapongeza viongozi mbali mbali wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, wafanyabiashara, madereva wa vyombo vya abiria vya usafiri wa nchi kavu na baharini pamoja na madaktari na wataalamu wa afya ambao tangu yalipoanza maradhi ya COVID-19 wamekuwa wakitoa huduma na elimu kwa wananchi.Alhaj Dk. Shein alivipongeza vyombo vya habari kwa kufanya kazi kubwa ya kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu maradhi hayo na kuwahimiza waendeleze ari na uzalendo wa kuyalinda maslahi ya nchi kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.

Rais Dk. Shein alitoa pole kwa wananchi wote waliopata msiba kwa kuondokewa na ndugu na jamaa zao kutokana na maradhi ya COVID-19, na kumuomba Mwenyezi Mungu awape subira na wale wote waliokwishatangulia mbele ya haki kutokana na maradhi hayo, Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema peponi.Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kuendelea kusherehekea siku hii ya Idd El Fitr kwa kwa kufanya mambo mema ya halali, pamoja na kuombeana dua za kheri zikiwemo zile za kuwaombea wagonjwa waliomo majumbani na hospitalini.

Alhaj Dk. Shein aliwataka Waislamu kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambayo yote yamefungamana na ucha mungu pamoja na kuyaendeleza na kuyadumisha wakati wote katika maisha yao na yasiwe katika Mwezi wa Ramadhani pekee yake.“Natoa salamu zangu kwa wananchi wote wa Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Waislamu duniani kote”  Dk. Shein alieleza katika salamu hizo.Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi na walezi kuendelea kusimamia malezi, usalama na afya za watoto katika Sikukuu hiyo ya Idd El Fitr ambapo viwanja vya kufurahishia watoto vimefungwa.

Aliwataka wananchi kujiepusha na husda, chuki na uhasama kwa visingizio mbali mbali ambapo mara nyingi mambo hayo husababishwa na kibri, dharau na kejeli miongoni mwa wanaadamu ambazo hizo ni khulka mbovu zinazoletwa na ushawishi wa shetani.Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa pole kwa wananchi wote waliokumbwa na mafuriko na hasa wale ambao nyumba na mali zao zimeathiriwa kutokana na mvua zilizonyesha.

Alieleza kuwa hivi sasa Serikali inaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote Unguja na Pemba yaliyoathirika ili iweze kurejesha miundombinu iliyoharibika na kuchukua hatua za haraka ili ione namna inavyoweza kuwahudumia walioathirika.Dk. Shein aliwahimiza wakulima kuitumia vyema neema ya mvua na kuzidisha nguvu katika kilimo cha mazao mbali mbali pamoja na miti ya kudumu ili kuimarisha mazingira pamoja na kuongeza upatikanaji wa chakula nchini.

Vile vile, Alhaj Dk. Shein aliipongeza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa jitihada zao za kuwasambazia maji wananchi katika kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa wale wote waliokuwa hawapati huduma hiyo.Pia, aliwahimiza viongozi wa Mamlaka hiyo kuhakikisha kwamba miradi mikubwa ya maji safi na salama iliyotekelezwa kwa ufanisi hivi karibuni inatoa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

Rais Dk. Shein aliendelea kuwahimiza na kuwakumbusha wafanyakazi wote walioko kwenye ajira ya Serikali na katika sekta binafsi, kuithamini na kuishukuru neema ya kupata ajira kwa kutekeleza dhamana na majukumu waliyokabidhiwa kwa uadilifu kwa kuzingatia sheria na kanuni mbali mbali zinazowaongoza.