Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaridhika na jinsi Shirika la Kimataifa la ‘Amref Health Africa in Tanzania’ linavyotekeleza vyema miradi yake hapa Zanzibar. 

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Kimataifa la ‘Amref Health Africa in Tanzania’ chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Dk. Florence Temu.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Shirika hilo limekuwa likifanya kazi nzuri na kuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya afya.

Alisema kuwa miradi mbali mbali inayofanywa na Shirika hilo hapa Zanzibar imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika uimarishaji wa sekta ya afya na matokeo yake yameonekana kuwa ni mazuri katika jamii.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba juhudi zaidi zinahitajika katika kuwashajiisha wananchi katika suala zima la chanjo ya UVIKO 19 sambamba na mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la ‘Amref Health Africa in Tanzania’ Dk. Florence Temu alimueleza Rais Dk. Mwinyi shughuli zinazofanywa na Shirika hilo hasa katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya afya hapa Zanzibar.

Dk. Temu alimueleza Rais Dk. Mwinyi jinsi wanavyotoa huduma kwa jamii kwa upande wa Zanzibar wakiwa kama wadau wa maendeleo ambapo wana miradi kadhaa ambayo wanaitekeleza kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Taasisi zake.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Shirika la Kimataifa la ‘Amref Health Africa in Tanzania’ lilimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake na kumkabidhi zawadi.