Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein,ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya kumuweka Wakfu Askofu wa 10 wa Dayosisi ya Zanzibar, Askofu Michael Henry Hafidh.
Alisema kuwa ustawi wa dini mbali mbali Zanzibar unahusika na Sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uhuru wa kuachia makanisa kuendesha seminari zao na makongamano yao bila ya kuingiliwa.
Alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa shughuli hizi za kidini zimekuwa zikiendeshwa kwa amani ambapo kwa bahati mbaya pamoja na hayo kumekuwepo nyakati ambapo kutofahamiana kumejitokeza katika baadhi ya makongamano.
“Serikali imeweka utaratibu maalum wa utoaji ruhusa wa makongamano hayo, taratibu hizo ni pamoja na utunzaji wa amani na kutobughudhiana kidini… tuelewe sote kwamba viongozi wa dini ni walimu na walezi wa jamii na wanadhamana kubwa mbele ya MwenyeziMungu”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kufanya kila linalowezekana kulinda haki za Watanzania katika kufuata dini na kuabudu dini waitakayo na kuishi bila ya kubaguliwa kutokana na sababu ya dini, kabila au rangi.