RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Saba ilifanya juhudi za makusudi katika kulibadilisha zao la karafuu kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) ili liende na wakati uliopo.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa kiwanda cha kusarifu majani makavu na yaliyoanguka wenyewe ya mkarafuu, huko Mgelema Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pembaambacho kimejengwa kwa mashirikiano ya Shirika la ZSTC pamoja na Kampuni ya Indesso kutoka ncini Indonesia.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa hivi sasa Shirika la ZSTC linakwenda kwa mabadiliko ya biashara na matumaini yake ni kwamba Awamu ya Nane ijayo itayaendeleza.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Saba iliongeza bei za zao la karafuu kutoka 3500 hadi kufikia 14,000 huku ikisisitiza kuwa hata soko la dunia likishuka basi Serikali itaendelea kuwalipa wakulima kwa bei hiyo hiyo ambayo inayoendela hadi leo.
Aliongeza kuwa uwekezaji huo ni uhusiano na ushirikiano mwema kati ya Zanzibar na Indonesia.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kujenga kiwanda hicho kwa lengo la kufahamu kuwa Mgelema na Ngomeni ni nguzo kubwa ya uzalishaji wa zao la karafauu.
Rais Dk. Shein alisema kuwa katika kuhakikisha uimarishaji wa zao la karafuu pamoja na bidhaa zake zinaimarika katika eneo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kazi ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Alisema kuwa tayari Serikali imeshajenga barabara ya Ngomeni pamoja na kupeleka kituo cha afya, umeme pamoja na huduma nyengine hivyo, baada ya miezi miwili barabara ya kutoka Kipapo hadi Mgelema itajengwa na kuahidi kuwa maisha ya wananchi wa kijiji hicho yatabadilika.
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia fupi ya zao la karafuu pamoja na biashara yake kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 na baada ya Ma[pinduzi hayo.
Katika maelezo yake hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar ndio waliopanda mikarafuu lakini wao hawakunufaika na zao hilo na badala yake walinufaika watawala waliotoka nje kuja kuitawala Zanzibar.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa bado karafuu ya Zanzibar inatakiwa na inapendwa kwani bado soko lake lipo na tayari hivi sasa karafuu imerudi hadhi yake ambapo hata magendo ya karafuu yamepungua kwa asilmia 5 na kuonesha wazi kwua hayapo.
Alisisitiza kuwa jumla ya tani 33,549.8 za karafuu kavu zenye thamani ya TZS Bilioni 448.684 zimenunuliwa kutoka kwa wakulimma katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2019 na jumla ya tani za karafuu 32,142.17 zenye thamani ya dola za Kimarekani 297,707,844 sawa na TZS Bilioni 553.89 zimeuzwa nje ya nchi.
Rais Dk. Shein aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 9 mfululizo Serikali ilimpa mkulimma kiwango cha asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la dunia ambayo ni sawa na TZS 14,000 kwa kilo moja ya karafuu kavu za daraja ka kwanza.
Nae Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina SalumAli alisema kuwa kiwanda hicho kitachangia kwa kiasi kikubwa kipato kwa wananchi hasa vijana kwani ndio wanaojishughulisha kwa kiasi kikubwa na shughuli za kiwanda hicho.
Balozi Amina alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kiwanda hicho ambacho kimetokana na ziara yake ya Kiserikali aliyoifanya nchini Indonesia mnamo mwezi wa April mwaka 2018.
Akitoa taarifa za kitaalamu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Juma Hassan Reli alisema kuwa kiwanda kitakuwa na uwezo wa kusindika kilogramu 250 za majani makavu kwa wakati mmoja na kutoa lita 7 za mafuta ambapo kitakuwa kikifanya kazi kwa mud a wa amasaa 24 na hivyo kuwezesha kupatikana lita 21 za mafuta kwa siku.
Mapema Balozi wa Indonesia Dk. Ratlan Pardede alisema kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho unaonesha uhusiano mwema na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia.
Alieleza kuwa tayari kwianda hicho kimeshaanza kuzalisha mafuta ya majani ya karafuu na kusisitiza kwua uzinduzi wa kiwanda hicho ni wmanzo tu na badala yake viwanda hivyo vitaendelea kujengwa Unguja na Pemba.
Alisema kuua kuansihwa kwa kwianda hicho kunajumuisha uhamasishaji wa teknolojia na kufungua uwezekano mwengine katika sekta nyengine.
Mwakilishi wa Kampuni ya Indesso kutoka Indonesia Feri Augusta alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano mazuri aliyoyapata na kusisitiza kuwa Kampuni yake itaendeleza kiwanda hicho sambamba na kuanzisha vyengine kwa manufaa ya nchi pamoja na wananchi hasa wale wanaokaa katika maeneo wanaoishi.
Mkuu wa Kampuni hiyo akitoa salamu kupitia video maalum akiwa nchini Indonesia alisema kuwa Kampuni yake itaendelea kutoa ushirikiano wake na Zanzibar kwani inathamini uhusiano uliopo pamoja na juhudi za Rais Dk. Shein anazozichukua.
Alisema kuwa anathamani mashirikiano hayo ya pamoja yaliopo ambayo yaliimarika zaidi pale Rais Dk. Shein alipofanya ziara yake ya Kiserikali nchini humo.
Katika uzinduzi huo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi mbali mbali.
Uzinduzi huo ulipambwa na ngoma mbali mbali kutoka kwa wasanii wa kiwani Pemba ikiwemo ngoma ya kibati pamoja na burudani nzuri ya nyimbo za Indonesia iliotumbuizwa na Putri Marsha Amanda na mwenziwe Ni Waga Supriani kutoka Bali, nchini Indonesia na nyimbo yao hiyo ya utamaduni maarufu ya Puspanjali.